Wakati mwili wa Frank Kapange ukifikisha siku ya 157 katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, gharama ya kuhifadhia mwili huo hospitalini hapo imefikia Sh3,140,000.
Frank alifariki dunia Juni 4, huku kifo chake kikigubikwa na utata uliodaiwa kutokana na mazingira ambayo ndugu hawakubaliani nayo.
Ndugu hao wanadai alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido na kwamba alikufa kutokana na kipigo alichopata akiwa mikononi mwa polisi jijini Mbeya.
Ndugu waligoma kuchukua mwili wake kwenda kuuzika wakisubiri hadi hatima ya rufaa waliyoiwasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya isikilizwe.
Ndugu wa familia hiyo chini ya wakili wao, Moris Mwamwenda waliliambia Mwananchi juzi kuwa wanasubiri hatima ya rufaa yao wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya iliyotupilia mbali maombi waliyoyawasilisha wakiiomba kutoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina juu ya sababu za kifo cha ndugu yao.
Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank uchukuliwe na ndugu ili wauzike, baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo chake, baada ya kuridhika na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawikili wa upande wa Serikali.
Hata hivyo, ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo, hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu.
Social Plugin