WATOTO WAWILI WAUAWA KWA KUCHINJWA BUKOBA


Mazishi ya watoto waliouawa yakifanyika

Watoto wawili, Auson Respicius (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Mashule na Alistidia Respicius (5) mwanafunzi wa chekechea katika shule hiyo wameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Mashule kata Kyamulaile wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kagera Issack Msengi alisema kuwa tukio hilo limetokea baada ya watoto hao kutoonekana nyumbani kwao kabla ya miili yao kuokotwa wakiwa wameuawa. 

Akielezea kuhusu tukio hilo,alisema watoto hao waliondoka nyumbani kwao siku ya Jumapili wakielekea katika maduka ya kijiji hicho na kuwa miili yao ilipatikana kesho yake siku ya Jumatatu Oktoba 22,2018 ikiwa katika shamba la migomba na iligundulika kuwa wamekatwa shingo na vitu vyenye ncha kali. 

“Mauaji haya yanahusishwa na imani potofu za kishirikina, kabla ya hili tukio bibi wa watoto hawa alituhumiwa kwa uchawi wananchi wakajichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba, inawezekana tukio hili ni ishara ya kuwataka wahame kijiji hapo” alieleza Msengi. 

Alisema tayari watu tisa ambao hawajatajwa majina yao kwa sababu za kiuchunguzi wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watoto wawili wa familia moja, waliouawa kwa kuchinjwa na watu ambao bado hawajafahamika. 

Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa watoto hao Respicius John alisema kuwa saa kumi jioni siku ya Jumapili aliwaandaa watoto wake na kuwavalisha nguo safi na kisha kuwaruhusu kwenda kutembea na watoto wenzao lakini hawakuonekana ndipo juhudi za kuwatafuta kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji zikaendelea. 

Kufuatia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Bukoba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Deodatus Kinawiro alimwagiza mkuu wa polisi wa wilaya ya Bukoba (OCD) Babu Sanale kufanya uchunguzi wa kina katika kijiji hicho na kuhakikisha wahusika wanakamatwa. 

“OCD nakuagiza fanya kazi usiku na mchana na hakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali, serikali haiwezi kukubali kuendelea kwa matukio haya ya kikatiri dhidi ya watoto tena ambao ni malaika hawajamkosea mtu yeyote” alisema.

Na Mwandishi wa Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم