Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na Kikosi 842 cha Jeshi Kujenga Taifa (JKT) Mlale, alipofanya ziara ya kikazi kuona shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na kikosi hicho.
Mkuu wa Kikosi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale, Luteni Kanali Al Solomon Shausi akielezea miradi ya uzalishaji mali iliyopo kwenye kambi hiyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi kuona shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na kikosi hiko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kutoka kwa Mwendesha Mitambo ya Kiwanda SG. Vereranda Kihali jinsi shughuli ya uchakataji sembe inavyofanyika katika kiwanda hiko, alipotembelea kambi ya JKT Mlale 842 kujionea shughuli za uzalishaji mali katika kambi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimjulia hali mtoto Hawa Mapunda, aliyelazwa (kulia) ni mama wa mtoto Bi. Christer Ndomba alipotembelea wodi ya watoto katika kituo cha afya cha JKT Mlale, Peramiho, akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jambo na Mkuu wa Kikosi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale, Luteni Kanali Al Solomon Shausi, alipotembelea kambi hiyo iliyopo Mlale, Peramiho Mkoani Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi mashuka kwa viongozi wa kambi ya JKT Mlale, alipofanya ziara kwenye kambi hiyo kujionea shughuli za uzalishaji mali.
Baadhi ya wanakikosi cha JKT 842 Mlale wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipowatembelea kambi hiyo kujionea miradi mbalimbali ya kikosi hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akipanda mti katika eneo la Kiwanda cha uchakataji sembe alipofanya ziara kambini hapo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wanakikosi alipokagua mmoja ya shamba la kikosi hiko wakati wa ziara kambini hapo.
Muonekano wa Kiwanda cha Uchakataji sembe katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Mlale.
NA MWANDISHI WETU:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amepongeza kazi za uzalishaji mali katika kambi ya Mlale.
Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi kwenye kambi hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Mlale kwa lengo la kuzungumza na kuangalia miradi mbalimbali ya uzalishaji mali kambini hapo.
Waziri Mhagama alisema kuwa dira ya taifa kufikia 2025 ni kuongeza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii kufikia hadhi ya uchumi wa pato la kati kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati hapa nchini inayolenga kuleta maendeleo ya wananchi na Taifa.
“Miradi hii iliyoanzishwa hapa imekuwa na tija kubwa kwa jamii iliyokaribu katika kufanikisha upatikanaji wa ajira kwa vijana na kukuza uchumi na maendeleo ya wanamlale na watanzania kwa ujumla” alisema Mhe. Mhagama.
Aliongeza kuwa, mageuzi ya kikosi cha JKT Mlale 842 yamekuwa ni makubwa sana hususan katika kuunga mkono maagizo ya Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata sembe kwa uwezo mkubwa na kuzalisha tani 440 kwa mwezi.
Aidha, Mheshimiwa Mhagama alihamasisha kikosi hicho kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana ikiwa ni njia moja wapo ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwezesha vijana kupata mafunzo ya stadi za kazi yatakayowawezesha kupata ujuzi wa kuweza kujiajiri na kuajiri.
Naye, Mkuu wa Kikosi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale, Luteni Kanali Al Solomon Shausi alieleza faraja waliyonayo kwa kutembelewa na Waziri katika kikosi hiko, kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kuahidi kuendelea kuimarisha kikosi katika matumizi ya ardhi na kutoa ushirikiano kwa wananchi ambao watakuwa tayari kujifunza hasa mambo ya kilimo cha umwagiliaji.
Wakati wa ziara hiyo ya kikazi Waziri Mhagama alitembelea Kiwanda cha kuchakata sembe cha kikosi hicho, Mashamba ya kahawa, shamba la mahindi, matikiti maji na matango, vilevile shule ya msingi ya Mlale na alichangia kiasi cha milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu, na kukabidhi mashuka kwa ajili ya kituo cha afya cha kambini hiyo iliyopo Jimbo la Peramiho, Mkoa wa Ruvuma.
Awali Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza mkakati wa kukuza ujuzi pamoja na program ya kitaifa ya kukuza ujuzi ya miaka mitano (2015/2016 hadi 2020/2021). Programu inalenga kuwezesha nguvu kazi ya taifa kupata ujuzi stahiki unaohitajika katika soko la ajira.
Hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kuwapatia mafunzo ya stadi za kazi vijana waliopo nchini kupitia programu hiyo.
Social Plugin