Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Jimbo lake kutoulizia Milioni 50 za kila kijiji ambazo ziliahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo Serikali imetoa milioni 800 kwa ajili ya kujenga hospitali za Tarafa katika baadhi ya kata kwenye jimbo hilo pamoja kupatiwa bilioni 2 kwa ajili utekelezaji miradi ambayo itawanufaisha wananchi wote.
Katika mkutano wake wa hadhara jimboni kwake, Mwigulu amesema; “nisikilizeni wana Iramba, Serikali imetupatia milioni 800 za kujenga hospitali za Tarafa Kinampanda na Ndago, tumepata zaidi ya bilioni 2 kujenga daraja tarafa ya Shelui, tumeshapata zaidi ya bilioni 2 kwa ajili ya maji.
"Hizi ni huduma za watu wote na hazikuwepo kwenye ilani, ni upendo na maono ya Rais. Tumshukuru mhe Rais wetu mpendwa badala ya kuulizauliza milioni 50. Na kwa Vikundi tutaendelea kuwapa asilimia kumi ya mapato ya ndani."
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi aliahidi kutoa milioni 50 kwa kila kijiji kwa nchini kwa ajili ya maendeleo.
Social Plugin