Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amezungumzia kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo) na kusema chama chao kimehangika sana kushughulikia tukio hilo, hivyo watu waache nongwa kwakuwa matukio ya uhalifu yanatokea duniani kote.
“Unajua watu waache nongwa, matukio haya ya uhalifu yapo duniani kote, sisi tumehangaika sana kama chama. Wametekwa watu Afrika Kusini hili si jambo la mzaha, watu wanatekwa kweli, kwa mfano Uingereza wametekwa watu miaka nane hawajarudi na polisi wanasema wanafamilia wasizungumzie hii kuonyeshwa kwamba huyo mtu hajarudi,” alisema Polepole.
Alisema kwa Tanzania kumetokea matukio mbalimbali yakiwemo ya mauaji ya watu katika wilaya za Kibiti na Mkuranga.
“Hapa kwetu tumepata shida mara kadhaa Mkuranga na Kibiti, hili jambo sisi ambao tupo katika uongozi wa chama na Serikali tunaona mzigo mzito, bahati mbaya wenzetu wanafanya mzaha kwenye mambo haya makubwa,” alisema Polepole.
Alisema kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha ulinzi unaimarika, hivyo inapotoea mtu ametekwa wao ndio wana kazi ya kufuatilia na kuchimbua kitaalamu kwa kushirikiana na wenzao wa kimataifa.
Polepole alisema Watanzania wamepiga maombi na dua kuhakikisha Mungu anawezesha kila chombo kinachofanya kazi kihakikishe Mo anarudi akiwa salama na kabariki ikafanikiwa, lakini cha kushangaza wapo watu wanaodai kuwa mfanyabiashara huyo hakutekwa.
“Mo amerudi anatokea mpuuzi anasema haaa, haaa Mo hakutekwa, mbona hawakumkata vidole. Sasa wakati tunaomba Mungu mlikuwa mnategemea nini? Unasema basi ndiyo kiongozi huyo amechaguliwa na watu.
“Baadhi ya watu hao walioomba kuingia CCM wasahau tu, hatutachukua watu ambao wanashindwa kuwa na utaratibu, wanashindwa kuelewa wanatamani watu wengine wapate tabu ili waamini kweli ilikuwa tabu,” alisema Polepole.
Alisema kitendo cha Mo kurudi bila kupata madhara yoyote ni cha kumshukuru Mungu, na Serikali ya CCM wamevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi mchana na usiku kuhakikisha wote wanaofanya vitendo hivyo wanapatikana.
“Wakipatikana washughulikiwe ipasavyo na kufanywa vitendo vyote vibaya kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wote ambao wanataka kufanya mchezo na spidi kubwa ya maendeleo ambayo tunaileta katika taifa letu la Tanzania,” alisema Polepole.