MUUZA GONGO KIZIMBANI KWA KUMHONGA ASKARI POLISI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imempandisha kizimbani mkazi wa Kijiji cha Kikatiti, Warieli Mungure, anayeuza pombe haramu aina ya gongo kwa tuhuma za kutaka kumhonga Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kikatiti, Marco Magere.



Katika shauri hilo namba 318 la mwaka huu lililopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, mtuhumiwa huyo alisomewa shtaka la kutoa hongo ya Sh 100,000 kwa Marco ili asimchukulie hatua za kisheria baada ya kuhusishwa na vitendo hivyo vya uuzaji pombe hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi, mtuhumiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Gwanta Mwankuga, Oktoba 10, mwaka huu.


“Mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 15(1) (b) na (2) cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kuzuia na kupambana na rushwa,” alidai.


Pia alisema walipata taarifa kutoka kwa Marco kuwa Mungure alimuahidi kuwa atakuwa akimpatia fedha hizo kila mwezi ili asifuatiliwe katika biashara yake.


Alisema baada ya kupata taarifa hiyo, walianzisha uchunguzi wa awali na baada ya kuthibitisha tuhuma waliandaa mtego Oktoba 9, mwaka huu uliofanikisha kumkamata Mungure katika eneo la Enspall Lodge, Kikatiti.


“Takukuru inawataka viongozi na watu wengine kuiga mfano wa Marco ambaye hakuwa tayari kuhongwa kwa sababu ni watu wachache wenye tabia hiyo ya kizalendo na tunawahakikishia taarifa zinazopokelewa zitafanyiwa kazi kwa haraka,” alisema.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 8, mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa huyo yuko nje kwa dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post