Msanii wa muziki wa Bongo fleva Emmanuel Elibariki maarufu kama 'Nay wa Mitego',amekanusha uvumi kuhusiana na kauli yake ya 'Zote kwa John' iliyopo katika wimbo wake mpya wa "ALISEMA" kuwa alimlenga Rais John Pombe Magufuli.
Akipiga stori na www.eatv.tv Nay amesema ametumia tafsida ya John kumuonesha kiongozi anayefanya mambo mazuri kwa jamii yake na pia anaweza kulaumiwa endapo atakiuka maadili katika kuwatumikia wananchi wake.
"Kwa sasa John ndio anaye laumiwa,ukizungumza mazuri ya John basi zungumza na mabaya yake pia kama binadamu anavyotenda mema na mabaya, hawezi fanya mazuri peke yake, sitaki kusema John gani, mimi ni msanii, natumia sanaa yangu kuweka mafumbo ili kufikisha ujumbe kwa hadhira, ukweli naujua mimi ambaye nimemuongelea", amesema Nay wa Mitego.
"Huu ni wimbo ambao una tafsiri nyingi sana, unahitaji utulize akili, unahitaji uwe na mawazo mapana ili uelewe,unahitaji ujiulize je ni wangu? au unanihusu mimi?, nafikiri nimejaribu kutumia tafsida na akili nyingi ili kila mtu anaye usikiliza aweze kutoka na tafsiri yake", ameongeza Nay.
Pia Nay wa Mitego amesema wimbo huo umemletea sifa nyingi baada ya kupokea simu za pongezi kutoka viongozi wengi hapa nchini na simu iliyo mshtua ni kutoka kwa kiongozi BASATA.
"Tangu nilipoachia wimbo huo nimepokea simu nyingi kutoka kwa viongozi wengi na wengine kutoka serikalini wakinipongeza, lakini simu iliyonishtua ni kutoka kwa kiongozi wa BASATA akaniambia sizungumzii BASATA ila nimekupigia simu kukupa pongezi ya wimbo wako mimi kama mimi binafsi nimeupenda, nilifurahi sana kusikia hilo, ila mpaka sasa sijapokea simu kutoka kwao".
Social Plugin