Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limefuta matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya shule ya msingi baada ya kubainika kuvujisha mtihani huo uliofanyika Septemba 5 na 6, 2018.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 2, 2018 amezitaja shule zilizofutiwa matokeo ni za halmashauri ya Chemba, Kondoa mkoani Dodoma.
Zingine ni Hazina na New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za jijini Dar es Salaam na Alliance na New Alliance na Kisiwani zote za Mwanza.
Dk Msonde amesema baada ya uchunguzi shule hizo zimebainika kuvujisha mitihani hiyo iliyofanyika Septemba 5 na 6 wakishirikiana na waratibu wa elimu wa eneo husika.
Akizungumzia wilaya ya Chemba, Dk Msonde amesema uongozi wa idara ya elimu ya halmashauri hiyo ulipanga kufanya udanganyifu kupitia waratibu wa elimu na wasimamizi kuhakikisha ufaulu unaongezeka.
"Uongozi uliandaa makundi ya ‘WhatsApp’ yaliyojulikana kama jina elimu Chemba, sayansi na hesabu na wasimamizi wa elimu Chemba. Makundi haya yaliwajumuisha waratibu wa elimu kata na baadhi ya wakuu ili kurahisisha mawasiliano baina yao,” amesema
Na Bakari Kiango,Mwananchi
Social Plugin