NB-Picha haihusiani na habari hapa chini
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma imemkamata Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma, (UDOM) Jacob Paul Nyangusi kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono.
Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Sosthenes Kibwengo amesema leo Oktoba 4, 2018 kuwa mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza ili amsaidie katika mitihani ya marudio aliyofanya hivi karibuni.
Amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Amesema mhadhiri huyo alikamatwa jana saa 3.00 usiku katika eneo la Nyumba 300 kata ya Nzuguni jijini hapa akiwa chumbani na mwanafunzi huyo.
“Awali, Takukuru ilipokea taarifa za mhadhiri huyo kutaka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake ambaye jina tunalihifadhi kwa sasa ili amwezeshe kufanya mitihani ya marudio baada ya kufeli na pia amsaidie wakati wa usahihishaji,” amesema.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo, Takukuru ilifanya uchunguzi wa awali na kuandaa mtego uliofanikisha kukamatwa kwake.
“Takukuru inaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kikitolewa,” amesema.
Amesema Takukuru mkoa wa Dodoma imekuwa ikipokea taarifa za baadhi ya wahadhiri wasio waadilifu kuwataka wanachuo hasa wa kike kingono ili wawasaidie katika masomo yao.
Amesema baadhi wamekuwa wanawafelisha wanafunzi kwa makusudi na baadaye kuwataka rushwa ili warekebishe matokeo yao.
Amesema wapo baadhi ya wahadhiri ambao baada ya kuwataka wanafunzi kingono na kukataliwa hutafuta namna ya kuwafelisha ili kuwakomoa.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Social Plugin