Ikiwa imetimia takribani miezi 10 tangu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi kuzuiwa kusafiri nje ya nchi baada ya Idara ya Uhamiaji kushikilia pasipoti yake, idara hiyo imesema inaendelea na uchunguzi wa uraia wake.
Uhamiaji imetoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu askofu huyo aliposema hawezi kusafiri nje ya Tanzania kutokana na kuwapo kwa zuio la mamlaka ya nchi tangu Desemba 2017 alipoanza kuhojiwa kuhusu uraia wake.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu uchunguzi wa uraia wa Askofu Niwemuguzi jana, msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda alisema, “Uchunguzi bado unaendelea tutakapokamilisha tutamjulisha mhusika.”
Alisema kwa kawaida uchunguzi wa uraia unapofanyika, “Huyo tunayemhofia tunamtaka kuwasilisha pasipoti yake kwa sababu pasipoti hutolewa kwa raia wa Tanzania, sasa unapokuwa unatiliwa shaka lazima tuichukue.”
“Lakini tutakapokamilisha uchunguzi na kubaini ni Mtanzania tunamrudishia na kama tutabaini si Mtanzania, tutamtaka sasa afuate taratibu zingine zikazomwwezesha kuishi nchini.” Miongoni mwa wanaochunguzwa uraia wao hadi sasa ni pamoja na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze; Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo.
Mtanda alisema, “Hata uchunguzi wa Eyakuze na Askofu Kakobe unaendelea na pasipoti zao tunaendelea kuzishikilia na Nondo kama naye alikuwa nayo basi tunaishikilia.”
Alisema uchunguzi wa uraia huwa hauna muda mwafaka kuwa utakamilika wakati gani.
“Uchunguzi mwingine huhusisha nje ya nchi, kwa hiyo mara tutakapokuwa tumekamilisha tutawajulisha wahusika.”
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi