Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Jeshi la polisi mkoani Kigoma limekanusha taarifa zilizotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, akisema kuwa Polisi mkoani humo wameua wananchi 100 katika tukio la kuwahamisha wakulima katika eneo la Mpeta.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kigoma,Maltin Otieno , amesema tarifa hizo ni za upotoshaji mkubwa na linatengeneza uhasama mbaya baina ya jeshi la polisi na raia.
Alisema Jeshi la polisi likiwa katika harakati ya kuwahamisha wafugaji katika eneo la Nalco katika Kijiji cha Mpeta Wilayani Uvinza, tukio lililotokea ni la askari wawili kuuawa ambao ni Ramadhani Mdimi na Mouhamed Nzengwe na wananchi wawili Sau Deusi na Adamu Baraka na majeruhi watano, na kwamba anashangaa kuona mwanasiasa huyo anadai jeshi la polisi limeua watu 100.
Hata hivyo Otieno alimuomba Kabwe kufika mkoani Kigoma na kuthibitisha taarifa anazozitoa kuhusiana na tukio hilo, na kwamba awapeleke katika eneo hilo ambao kuna wananchi wameuawa kwa kupigwa na polisi.
Aidha amewataka wanasiasa kutumia vizuri majukwaa ya siasa kuwahamasisha wananchi kujiletea maendeleo na siyo kutumia majukwaa kutoa taarifa za uongo, na jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua atakae jihusisha na upotoshaji wa suala hilo au jambo lolote.
Social Plugin