Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta ameendelea kutikisa ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, kwa kufungia klabu yake mabao mawili katika mechi iliyochezwa Alhamisi.
Aliisaidia klabu yake ya KRC Genk kuwalaza Besiktas wa Uturuki kwa mabao 4-2.
Katika mechi hiyo, langoni alikuwa kipa wa Liverool Loris Karius ambaye anakumbukwa kwa kufanya makosa makubwa na kuchangia Liverpool kushindwa kwenye fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei mwaka huu.
Samatta alifunga bao la kwanza dakika ya 23 na kisha akaongeza la pili dakika ya 70 baada ya kupokea mpira kutoka kwa Joakim Maehle nyakati zote mbili.
Mabao yote mawili aliyafunga kwa mguu wake wa kulia.
Besiktas walikomboa bao moja dakika ya 74 kupitia Vagner Loveawazisha dakika ya 74, lakini Genk wakaongeza mabao mengine mawili kupitia Dieumerci Ndongala (81') na Jakub Piotrowski (83).
Vagner Love alikombolea Besiktas bao jingine dakika ya 86 lakini hawakuwa na muda na mechi ikamalizika 4-2.
Samatta alikuwa amepiga krosi ambayo ilizalisha bao lililofungwa na Piotrowski. Aliondolewa uwanjani dakika ya 87 na nafasi yake akaingia Zinho Gano.
Sasa, nyota huyo wa Tanzania amefunga mabao matatu katika hatua ya makundi Europa League, ingawa alikuwa amefunga mengine matano mechi za muondoano za kufuzu za kabla ya hatua ya makundi.
Alifunga bao moja dhidi ya Malmo FF 20 Septemba, lakini hakufunga Sarpsborg 08 mnamo 4 Oktoba.
Katika mechi za kufuzu Europa League msimu huu, alifunga mabao mawili dhidi ya Lech Poznan, bao moja kila mechi.
Mnamo 23 Agosti 2018 Samatta, alifunga 'hat-trick' dhidi ya Brøndby IF katika Europa League kwenye mechi ambayo walishinda 5-2, na baadaye mechi ya marudiano akawafunga bao moja.
Taarifa kutoka Uingereza siku za hivi karibuni zimedokeza kwamba anatafutwa na klabu za West Ham United, Everton na Burnley kutokana na ustadi wake msimu huu katika kufunga mabao.
Via BBC
Social Plugin