Naibu Waziri wa TAMISEMI Josephat Kandege (kulia) Oktoba mosi, 2018 alifika Soko la muda la Kisutu, ilipokuwa Stendi Kuu ya kwanza ya mabasi ya kwenda mikoani. Wafanyabiashara hao wamepelekwa hapo kwa muda baada ya Manispaa ya Ilala kuamua kujenga Soko jipya la kisasa la Kisutu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala (MD) Jumanne Shauri akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa kwenye Manispaa hiyo ikiwemo Soko jipya la kisasa Kisutu ambalo litakuwa la ghorofa nne.
**
Na Yusuph Mussa - Dar es salaam
MANISPAA ya Ilala jijini Dar es Salaam inajenga Soko jipya la kisasa Kisutu ukiwa ni mradi utakaoweza kuleta ukombozi na kuifanya Manispaa hiyo kuendelea kuongoza kwa ukusanyaji mapato nchini.
Mradi huo unatarajia kukusanya sh. 259,860,400 kwa mwezi, huku kwa mwaka ukikusanya sh. 3,118,324,800, kitakuwa ndicho chanzo cha kwanza katika miradi ya Manispaa, na cha tatu katika vyanzo vya makusanyo ya ndani kwa Halmashauri ya Manispaa Ilala.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 28, 2018, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala (MD) Jumanne Shauri, alisema mradi unajengwa kwa gharama ya sh. 13,484,067,101, na fedha za ujenzi wa mradi huo ni ruzuku kutoka Serikali Kuu.
"Soko la kisasa linajengwa Kata ya Mchafukoge, Mtaa wa Kitumbini katika eneo ambalo lilikuwepo soko la zamani, ambalo lilikuwa na uchakavu mkubwa na miundombinu ya kizamani. Soko la Kisutu lilianzishwa mwaka 1964 likiwa na idadi ndogo ya wafanya biashara. Kwa sasa Soko la Kisutu lina jumla ya wafanya biashara 669 wa nje na ndani, ambapo inajumlisha wafanyabiashara 201 ni wa kuku hai na kuchinja, na wafanyabiashara wengine wa nafaka, mbogamboga na matunda jumla yao ni 468.
"Eneo la ujenzi wa soko la kisasa lina jumla ya mita za mraba 2,285. Soko hili linahudumia jamii kubwa kwani lipo katikati ya Jiji la Dar es salaam na lina bidhaa kama nafaka, matunda, mbogamboga, kuku hai wa kisasa na asili, huduma ya uchinjaji wa kuku, huduma ya mama lishe pamoja na vibanda vya huduma nyinginezo", alisema Shauri.
Shauri alisema, mradi unatarajiwa kutekelezwa ndani ya wiki 72, na soko hilo litakuwa la ghorofa nne (4) na sakafu ya chini na ya kwanza, ambapo sakafu ya chini ni kwa ajili ya maegesho na machinjio ya kuku, sakafu ya kwanza (ground floor) itakuwa maduka ya nyama, sehemu ya mabenki na biashara nyinginezo.
Alisema ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya nafaka, matunda na mbogamboga na bidhaa zote za chakula. Ghorofa ya pili ni wafanyabiashara wa bidhaa aina ya korosho na karanga, ghorofa ya tatu ni maduka makubwa na madogo ya biashara mchanganyiko zisizokuwa za chakula, pia ghorofa ya nne ni maduka makubwa na madogo ya biashara mchanganyiko zisizokuwa za chakula, na sehemu ya mwisho (roof floor) kwa ajili ya migahawa.
"Wafanyabiashara zaidi ya 1,500 kwenye soko hilo watanufaika ukilinganisha na wafanyabiashara wa sasa 669, kutakuwa na vizimba kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo, maduka makubwa (Mall) na madogo, maeneo ya machinjio ya kuku, mama na baba lishe, na biashara nyingine kulingana na mahitaji ya wakati huo kwa kuwa kutakuwa na maeneo ambayo yatapangishwa kulingana na ukubwa wa mita za mraba.
"Makadirio kwa mwezi tunatarajia sh 259,860,400, na kwa mwaka sh 3,118,324,800. Kitakuwa ndicho chanzo cha kwanza katika miradi ya Manispaa, ila cha tatu katika vyanzo vya makusanyo ya ndani kwa Halmashauri ya Manispaa Ilala. Litachukua zaidi ya watu 3,000 kwa wakati mmoja" alisema Shauri.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Selemani Jafo, hivi karibuni akiwasilisha Taarifa ya ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri zote nchini ya mwaka 2017/2018 akiwa jijini Dodoma, alisema Halmashauri zilizoongoza kwa kiwango kikubwa cha mapato nchini, ya kwanza ni Manispaa ya Ilala sh. bilioni 44.5, ya pili Manispaa ya Kinondoni sh. bilioni 29.7, tatu Manispaa ya Temeke sh. bilioni 29.4 na nne ni Manispaa ya Dodoma ni sh. bilioni 25.5.
Halmashauri zilizokusanya mapato kidogo nchini, ya kwanza ni Kakonko sh. milioni 347.1, ya pili Buhigwe sh. milioni 371.2, na tatu ni Kigoma sh. milioni 418.7.
Social Plugin