TCRA KUWASHUGHULIKIA WASANII WANAOSAMBAZA VIDEO ZA NGONO MTANDAONI


Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakanjala (kushoto) akiwa na Wema Sepetu.

Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), imesema Jeshi la Polisi kitengo cha makosa ya mtandaoni ndicho chenye jukumu la kuchukua hatua za kisheria kufuatia kusambaa mitandaoni kwa video za wasanii mbalimbali hapa nchini zenye maudhui ya kingono.

Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakanjala ameieleza East Africa Breakfast kuwa, kazi ya mamlaka hiyo ni kuelimisha kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Mwakanjala amesema kuwa, makosa yote ya jinai yakiwemo yale ya mitandao hushughulikiwa na jeshi la polisi na kwamba mamlaka hiyo inachoweza kufanya ni kutoa usaidizi wa kiuchunguzi na kiteknolojia tu kwa jeshi la polisi pale linapokuwa linashughulikia uhalifu huo.

"Sisi kazi yetu ni kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao, tukiwataka watumie kwa faida kwakuwa mitandao ya kijamii imerahisisha maisha, lakini makosa hayo hatushughuliki nayo bali yanasimamiwa na kitengo cha makosa ya mitandaoni chini ya jeshi la polisi", amesema Mwakanjala.

Video za wasanii watatu wa kike, zimesambaa mitandaoni tangu juzi, wasanii hao ni pamoja na mshindi wa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, na mwigizaji Wema Sepetu, Amber Rutty pamoja na Amber Lulu.

Tayari msanii Wema Sepetu na Amber Rutty wamejitokeza na kuomba radhi kutokana na kusambaa kwa video hizo, huku wakishindwa kufafanua mazingira ya kurekodiwa na hata kusambaa kwake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post