Mkurugenzi wa Famari Store Mohamed Abri (kulia) akijadili jambo la meneja wa wakala wa majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Iringa Fazes Tarimo wakati wa mafunzo hayo.
Kushoto ni Fundi rangi za majumbani kutoka mkoa wa Iringa akipewa maelekezo ya upakaji rangi kutoka kwa mkufunzi wa kampuni ya Slikcoat ya nchini Uturuki Saleh Ahmed jana wakati wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Famari Store ya mkoani Iringa kwa mafundi rangi zaidi ya 100
Wakala wa majengo Tanzania (TBA ) mkoa wa Iringa amepongeza kampuni ya Famari Store kwa kutoa mafunzo kwa mafundi rangi wa mkoa wa Iringa na Njombe kuwa yatasaidia kuongeza ubora wa majengo mkoani hapa.
Meneja wa TBA mkoa wa Iringa Fazes Tarimo ametoa pongezi hizo jana wakati akifunga mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na kampuni ya Famari Store ya mkoa Iringa na kuendeshwa na kampuni ya Slkcoat Print Co.Ltd ya nchini Uturuki kupitia tawi lake la jijini Dar es Salaam .
Alisema mafunzo hayo ni mazuri yanakwenda sawa na mpango wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli kuelekea uchumi wa viwanda na kuwa kupitia mafunzo hayo kutaongeza ajira kwa vijana na kuwa na vijana wenye ujuzi wa matumizi sahihi ya rangi .
Alisema anatumaini kuona ubora wa upakaji wa rangi katika majengo yanayoendelea kujengwa utazingatia sifa sahihi ya upakaji wa rangi pia kuwa na mafundi wenye utashi wa aina za rangi wanazotumia.
Mkurugenzi wa Famari Store ambao ni waandaaji wa mafunzo hayo Mohamed Abri alisema kuwa waqmekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya rangi na kuwa tayari wametoa mafunzo kama hayo ya uchanganyaji wa rangi na upuliziaji kwa mafundi magari na sasa ilikuwa ni zamu ya mafuni rangi za majumbani .
Abri alisema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa mafundi zaidi ya 100 kutoka mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani na kuwa lengo ni kuwa na mafundi wenye uelewa wa matumizi ya rangi .
Hivyo alisema wao kama mawakala wa rangi kutoka kampuni ya Slikcoat ya nchini Uturuki wameona ni vema kuwapa mafunzo mafundi hao ili kusaidia kurahizisha uuzaji wa rangi na kuwa na mafundi wenye uelewa wa kutosha ambao watajua ni rangi aina gani inapaswa kupagwa sehemu gani na namna ya kuichanganya na kuipaka.
Aidha alisema kuwa rangi hizo kutoka nchini Uturuki zimekuwa zikihitajika zaidi na suala ambalo wao wameliona ni baadhi ya mafundi kutokuwa na uelewa wa kuzitumia lakini kwa mafunzo hayo wanaamini mafundi hao wataweza kuwa wabobezi wa upakaji rangi .
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka kampuni ya Slikcoat Saleh Ahmed alisema kuwa mafundi hao wameweza kuonyesha uelewa wa kutosha baada ya kufanyiwa majaribio mara baada ya mafunzo hivyo ni imani yake kuwa na ubora zaidi katika kazi yao .
Wakishukuru kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo hayo Iren Mathias na Jonas Mbasa walisema kuwa kutolewa kwa mafunzo hayo kutawaongezea wateja zaidi na kuwa badala ya makampuni kuchukua mafundi rangi kutoka nje ya mkoa wa Iringa sasa watalazimika kununua rangi Iringa na kupata mafundi ndani ya mkoa.
Social Plugin