Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA WA MKONGE KOROGWE WAKUMBUSHA AHADI YA DKT. TIZEBA

Na Yusuph Mussa, Korogwe

BAADHI ya wakulima wadogo wa mkonge Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamemuomba Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Kizeba kukumbuka ahadi yake ya kushughulikia matatizo ya wakulima hao na Kampuni ya Katani Ltd ili kuruhusu shughuli za uzalishaji wa zao hilo uendelee.

Kwani baada ya kufanya ziara kwenye baadhi ya mashamba na viwanda vya mkonge Septemba 25, mwaka huu, alisema atashughulikia suala hilo ndani ya siku 14 ili kuruhusu uzalishaji uendelee, ambazo siku hizo zilikuwa zinaisha Oktoba 9, 2018.

Ni baada ya uzalishaji kwenye viwanda vinane (8) vya mkonge chini ya Katani Ltd kusimama tangu Agosti 21, mwaka huu baada ya Tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela kutoa mapendekezo kadhaa ikiwemo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua hesabu za kampuni hiyo na madai ya wakulima.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana (Oktoba  9) kwa nyakati tofauti kwenye Shamba la Mkonge Mwelya, wakulima walisema, kama wataendelea kukaa bila kufanya shughuli za uzalishaji wa mazao yao, wataathiri kwa kiwango kikubwa.

"Sisi tuna imani na Serikali yetu ya Awamu ya Tano na tuna imani na Waziri wa Kilimo. Tunaomba ile ahadi yake ya kuona anamaliza tatizo hili lililosababisha kufungwa kwa viwanda hili linakwisha. Na tangu ameahidi kushughulikia suala hili ndani ya siku 14, mwisho wake ni leo (Oktoba 9). Hivyo tunaamini atatoa majibu.

"Kufungwa viwanda hivi kwa zaidi ya miezi miwili sasa, athari zake ni kubwa. Moja ya athari hizo ni mkonge kuharibika ukiwa shambani, kwani baadhi ya mkonge huo umekomaa. Lakini kwa kushindwa kupata kipato, tunajikuta tunashindwa kupata mahitaji yetu kuanzia kusomesha watoto wetu na kupata chakula" alisema mkulima Mohamed Mgaya.

Mkulima Mariam Mussa alisema yeye ni mjane, lakini anategemea kuuza mkonge wake ili kumsomesha mtoto wake ambaye yupo Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro. Hofu yake, kama suala hili la kutafuta muafaka kati ya wakulima na Katani Ltd litaendelea kwa muda mrefu, wataumia wengi.

"Mimi ni mjane ambaye ili niweze kuendesha maisha yangu nategemea kuuza mkonge. Mkonge ndiyo unaniwezesha kupata fedha na kutimiza mahitaji yangu yote ikiwemo kumsomesha kijana wangu ambaye yupo Chuo Kikuu cha Mzumbe. Namuomba sio Waziri tu wa Kilimo hata Rais Dkt. John Magufuli atusaidie ili kumaliza mgogoro wetu kati ya Katani Ltd na wakulima.

Ernest Mhina alisema wizi wa kuvunjwa majumba mitaani umerudi tena, kwani vijana waliokuwa wameajiriwa kwenye mashamba hayo hawana kazi za kufanya, hivyo anaamini Waziri wa Kilimo atatimiza ahadi yake ya kuruhusu uzalishaji kwenye viwanda vya mkonge uweze kuendelea.

Kwenye mikutano ya kusikiliza kero za wakulima hao hivi karibuni, Shigela alisema moja ya maazimio ya Kamati aliyounda ni kuona maslahi ya wakulima yanalindwa. Moja ya maazimio hayo ni mgawanyo wa mapato kati ya Katani Ltd na wakulima, ambapo mwanzoni ulipendekezwa uwe asilimia 54 kwa Katani Ltd na 46 kwa wakulima, lakini baadhi ya wakulima wameulalamikia.

Maazimio mengine ni mkonge huo uuzwe kwa mnada, CAG aende akakague hesabu za Katani Ltd na wakulima, wakulima wakope fedha kwenye taasisi za fedha badala ya kuntegemea mtu mmoja kufanya hivyo yaani Katani Ltd. Na Katani Ltd ilipe malikimbizo ya madeni ya wakulima, huku wakulima wakitakiwa kulipa madeni wanayodaiwa na Katani Ltd na SACCOS.
Mashine ya kusindika mkonge (korona) kwenye Kiwanda cha Mkonge Mwelya wilayani Korogwe mkoani Tanga, ikiwa imesimama baada ya shughuli za uzalishaji kusimama kwa zaidi ya miezi miwili kwenye viwanda vinane (8) vya Kampuni ya Katani Ltd. Shughuli za uzalishaji zimesimama ili kupata muafaka wa kimaslahi kati ya Katani Ltd na wakulima wadogo. (Picha na Yusuph Mussa).
Vichanja vya kuanika mkonge (brashi) Kiwanda cha Mkonge Mwelya wilayani Korogwe mkoani Tanga, baada ya shughuli za uzalishaji kusimama kwa zaidi ya miezi miwili kwenye viwanda vinane (8) vya Kampuni ya Katani Ltd. Shughuli za uzalishaji zimesimama ili kupata muafaka wa kimaslahi kati ya Katani Ltd na wakulima wadogo. (Picha na Yusuph Mussa).
Trela za trekta kwenye Kiwanda cha Mkonge Mwelya wilayani Korogwe mkoani Tanga, zikiwa zimesimama baada ya shughuli za uzalishaji kusimama kwa zaidi ya miezi miwili kwenye viwanda vinane (8) vya Kampuni ya Katani Ltd. Shughuli za uzalishaji zimesimama ili kupata muafaka wa kimaslahi kati ya Katani Ltd na wakulima wadogo. (Picha na Yusuph Mussa).
Trekta na lori kwenye Kiwanda cha Mkonge Mwelya wilayani Korogwe mkoani Tanga, yakiwa yamesimama baada ya shughuli za uzalishaji kusimama kwa zaidi ya miezi miwili kwenye viwanda vinane (8) vya Kampuni ya Katani Ltd. Shughuli za uzalishaji zimesimama ili kupata muafaka wa kimaslahi kati ya Katani Ltd na wakulima wadogo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkonge ambao ndiyo daraja la juu kwa sasa (UG), ambao ulikuwa upo tayari kusafirishwa kwenda sokoni nchi za Ulaya na Marekani, ukiwa umehifadhiwa kwenye ghala la Kiwanda cha Mkonge Ngombezi kilichopo chini ya Kampuni ya Katani Ltd wilayani Korogwe mkoani Tanga. Mkonge huo ambao ni wa wakulima wadogo, umezuiwa kwenda sokoni mpaka muafaka upatikane kati ya Katani Ltd na wakulima wadogo. (Picha na Yusuph Mussa).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com