Na Yusuph Mussa, Korogwe
WAKULIMA wa mkonge wilayani Korogwe mkoani Tanga chini ya Mfumo wa Wakulima Wadogo wa Mkonge (SISO), wameeleza mafanikio waliyoyapata kwa miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mfumo huo na Kampuni ya Katani Ltd mwaka 1998.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Oktoba 13, 2018 kwa nyakati tofauti kwenye Shamba la Mkonge Mwelya, wamesema mafanikio waliyoyapata ni makubwa ukilinganisha kabla ya kuwa na kilimo hicho.
Mkulima Mohamed Mgaya alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mazao mengine kama mahindi hayakuweza kuwasaidia, lakini ujio wa kilimo cha mkonge cha kibiashara ambacho kilifanywa na mkulima mmoja mmoja, kimewainua kimaisha.
"Wakati tunaanza hali ilikuwa mbaya, lakini baada ya kupambana na kuimarisha, sasa hivi tunafaidi matunda yake, kwani tumejenga nyumba, tuna usafiri kama magari na bajaj kwa ajili ya biashara, lakini kabla ya hapo mimi nikiwa mstaafu serikalini, sikuwa hata na baiskeli", alisema Mgaya.
Mgaya alisema ni kweli kuna changamoto ndani ya mfumo wa SISO sasa hivi na Serikali imeingilia kati, lakini anaamini suluhu ya jambo hilo itapatikana muda si mrefu.
"Hapa katikati kumetokea ucheleweshaji wa malipo yetu kwa sisi wakulima ambao tumeingia mkataba wa kuiuzia mkonge Kampuni ya Katani Ltd, na jambo hilo kumfanya Mkuu wa Mkoa wa Tanga (Martin Shigela) kuingilia kati. Tunasema tuiombe Serikali ikamilishe mchakato wa kupata muafaka huo ili tuendelee na uzalishaji wa zao hili, faida tunayopata kwa kuwepo mfumo wa SISO ni kubwa kuliko hasara", alisema Mgaya.
Mkulima Ernest Mhina ambaye kilimo cha mkonge ameanza 2010, alisema mkonge umemfanya kuwa na uwezo wa kufanya mambo mengine, mfano ameweza kununua mashamba mengine kama ya mahindi, na kuongeza Serikali iwekeze kilimo hicho kwa kukiona kama ndiyo korosho kwa mikoa ya kusini na pamba ama madini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
"Nimeweza kusomesha wanangu, kununua mashamba ya mazao mengine kwa kutumia fedha za zao la mkonge. Jambo la muhimu Serikali ione umuhimu wa kurudisha haraka zao hili la mkonge ili tuendelee na uzalishaji", alisema Mhina.
Mariam Mussa, akiwa mjane, amesema mkonge ulikuwa kama mkombozi kwake, kwani pamoja na kumpa mahitaji yote muhimu, lakini umemuwezesha kumsomesha mtoto wake hadi Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, na hadi sasa anaelekea kumaliza, hivyo kwake mkonge ni mkombozi, kwani pia amejenga nyumba na kuweka umeme kwa fedha za kilimo cha mkonge.
Maurice Nkondokaya ambaye ni mmoja wa wakulima wakubwa wa mkonge kwenye Shamba la Mwelya akiwa na hekta 30 sawa na ekari 70, alisema baada ya kustaafu serikalini Idara ya Maendeleo ya Jamii kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mwaka 2009, mafao yake aliwekeza kwenye mkonge, na faida yake ameiona, kwani fedha anazopata ni nyingi na kumuwezesha kukidhi mahitaji yake.
Habiba Mbelwa ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Makuyuni alisema pamoja na matatizo yaliyopo ndani ya mfumo wa SISO, bado kuna faida kubwa wameipata kupitia kilimo cha mkonge, hivyo dhana ya uchumi wa viwanda, tayari kwao inatekelezwa, hivyo ni Serikali kuweza kuwasimamia waweze kufanikiwa.
"Wakulima tunakiri tumepata mafanikio kwa kuwepo mfumo huu wa SISO. Na tunapozungumzia uchumi wa viwanda, tayari sisi wakulima wa mkonge Mwelya tunavyo, tunachotaka ni Rais Dkt. Magufuli aweze kutilia mkazo sisi wakulima wa mkonge tusaidiwe. Tuna matatizo mengi ikiwemo mitaji midogo na ucheleweshaji wa malipo kwa wakati" ,alisema Mbelwa.
Viwanda vinane (8) vya mkonge chini ya Katani Ltd vimesitisha uzalishaji tangu Agosti 21, 2018 ili kupisha muafaka wa makubaliano ya maslahi kati ya Katani Ltd na wakulima. Ni baada ya Kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa Shigela kubaini kasoro kwenye mfumo wa SISO, na Kamati hiyo kutoa mapendekezo yake ambayo sasa ndiyo yanafanyiwa kazi.
Bidhaa zitokanazo na mkonge
Mkonge unatengenezewa bidhaa nyingi ikiwemo viti, mikoba, busati na meza.
Mkulima wa Mkonge Shamba la Mwelya wilayani Korogwe, Ernest Mhina akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata kwenye mfumo wa SISO.
Mkulima wa Mkonge Shamba la Mwelya wilayani Korogwe, Mariam Mussa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata kwenye mfumo wa SISO.
Mkulima wa Mkonge Shamba la Mwelya wilayani Korogwe, Maurice Nkondokaya akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata kwenye mfumo wa SISO. (Picha zote na Yusuph Mussa.
Social Plugin