Uongozi wa Kampuni ya ulinzi ya Ultimate inayolinda maeneo
ya Gymkhana jijini Dar es Salaam, umeeleza jinsi ambavyo askari wake
walifanikiwa kumpa msaada Mohammed Dewiji baada ya kutupwa na watekaji,
usiku wa manani, Oktoba 20 mwaka huu.
Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Eliuta Mwanjawike amesema kuwa walinzi
watatu wa kampuni hiyo waliokuwa zamu ndio waliofanikiwa kukutana na Mo
kwa mara ya kwanza baada ya kuachiwa na watesi wake.
Amesema kuwa walinzi wake walimuona mtu anayewafuata akieleza kuwa
anahitaji msaada, ndipo walipomwambia asimame alipo na kujieleza.
Mwanjawike aliyefanya mahojiano na Mwananchi amesema kuwa Mo
alijitambulisha kwa walinzi hao na kuwaeleza kuwa ndiye aliyekuwa
ametekwa na aliwaomba wampeleke katika hoteli ya Holiday Inn ili
awapigie simu wazazi wake.
“Askari wangu wakamjibu, Holiday Inn ni mbali, ila ngoja tukuitie
usafiri wa ofisi ukupeleke kwenye hoteli hiyo,” Mwananchi wanamkariri
Mwanjawike.
“Hata hivyo, Mo aliwaambia hadi gari la ofisi lifike watachelewa
hivyo aliwaomba wampeleke kwenye hoteli yoyote iliyo karibu na eneo
hilo,” aliongeza.
Alisema walinzi wake wawili kati ya watatu waliokuwepo walimpeleka
katika hoteli ya Southern Sun, iliyoko karibu zaidi na eneo (takribani
mita 210) hilo kwa kulinganisha na ilipo Holiday Inn.
Alisema kuwa walinzi hao walisubiri hadi ndugu wa Mo Dewji walipofika
na kumchukua katika hoteli hiyo, ndipo walipoondoka kurejea katika
kituo chao cha kazi.
Kwa mujibu wa Msemaji wa familia ya bilionea huyo, Azziz Dewji baada
ya kumfuata katika eneo hilo walimpeleka moja kwa moja nyumbani.
“Afya yake ni kamilifu kwa asilimia 100, labda tu saikolojia yake kidogo kutokana na tukio la kutekwa,” alisema Azziz.
Mo alitekwa Oktoba 11 katika hoteli ya Colosseum iliyoko Osterbay
jijini Dar es Salaam, alipokwenda kufanya mazoezi majira ya saa 11
alifajiri.
Social Plugin