Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AMWAGIZA WAZIRI WA MAJI KUKAGUA MIRADI YA MAJI KYERWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kwenda wilayani Kyerwa kwa ajili ya kukagua maendeleo ya miradi ya maji na endapo atabaini ubadhilifu achukue hatua kwa watakaohusika.


Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 7, 2018) baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilaya Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Mkewe Mama Mary Majaliwa.


“Waziri wa Maji na Umwagiliaji atakuja hapa kukakagua miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya hii na pale atakapobaini ubadhilifu achukue hatua.” Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi na mananchi wa wilaya hiyo baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa miradi ya maji.


Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya ya Kyerwa ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo kuliko kutafuta maji.


Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Amewataka wananchi nao kutunza vyanzo vya maji ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.


Amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma zote muhimu, hivyo amewataka waendelee kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaboreshea maendeleo katika sekta za afya, maji, elimu , miundombinu na kilimo.


Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa wa Kagera kuwahamasisha wananchi wake kujinga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF), ambao utawapa fursa ya kupatiwa huduma za matibabu wao na familia zao kwa mwaka mzima bure.


Awali, Mbunge wa jimbo la Kyerwa, Bw. Inoncent Bilakwate pamoja na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Kagera Bibi Oliver Semnguruka walimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika uboreshwaji wa huduma za maji na afya.


Bw. Bilakwate alisema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tatu katika jimbo hilo, lakini ujenzi wake hauridhishi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 7, 2018.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com