Bodi ya Filamu nchini, imemfungia msanii wa filamu 'Bongo Movie' Wema Sepetu, kutojishughulisha na masuala ya filamu kwa muda usiojulikana kutokana na picha zake za faragha/chafu kusambaa mitandaoni.
Akitoa uamuzi huo mbele ya vyombo vya habari, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Joyce Fissoo amesema kuwa Wema amekuwa akijihusisha mara kwa mara na matukio ya kusambaza picha zisizo na maadili mitandaoni na amekuwa akionywa na vyombo husika lakini amekuwa akirudia.
"Msanii wa filamu nchini Tanzania, Wema Sepetu leo baada ya kuitwa kuhojiwa na Bodi ya Filamu Tanzania kuhusu kusambaa kwa picha zake za faragha kwenye mitandao ya kijamii, na kwakuwa amekwisha onywa mara kadhaa safari hii tumeamua kumfungia kabisa kutojihusisha na mambo ya filamu", amesema Fissoo.
Ameongeza kuwa " Kitendo kile kimelidharirisha taifa, jinsia na mashabiki wake wameiga tabia baadhi kupitia video ile, hivyo basi kwakuwa amekiri na kuomba radhi kwa maandishi, atatumikia adhabu hiyo mpaka pale tutakapojiridhisha kuwa amebadilika".
Mapema jana Wema aliomba msamaha kutokana na tukio hilo ambalo lilitokea siku kadhaa nyuma ambapo ilimuonesha akiwa faragha na mwanaume anayesemekana ni raia wa Burundi, aliyedai kuwa ni mume wake mtarajiwa.
Chanzo- EATV
Social Plugin