ACT WAZALENDO YAINGILIA KATI SAKATA YA RUSHWA YA NGONO UDSM


Msemaji wa ACT - Wazalendo Ado Shaibu, na Dkt Vicensia Shule.

Wakati sakata la kukithiri kwa rushwa ya ngono katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) likishika kasi, Chama cha ACT-wazalendo kimeingilia kati na kutoa msimamo wake kuhusu suala hilo.


Taarifa hiyo ya ACT imesema imeshtushwa na taarifa inayosambaa mitandaoni mbalimbali ya kijamii kwamba mhadhiri wa chuo hicho na mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, Dkt Vicensia Shule ameitwa na Kamati ya Maadili ya chuo baada ya andiko lake katika mtandao wa Twitter kusambaa.

ACT imesema kuwa itasimama katika upande wa Dkt Vicensia endapo atakosa haki yake na kusisitiza kwamba kitendo kilichofanywa na Kamati ya Maadili ya chuo hicho si sahihi kwakuwa ilipaswa ichunguze juu ya ukweli wa taarifa hizo kabla ya kumuita.

"Chama chetu kinafuatilia kwa karibu juu ya suala hili na popote pale ambapo Dkt Shule ataonewa tutasimama naye. Kusimama na Vicensia ni kusimama na mtoto wa kike anayenyanyasika chuoni kwa rushwa ya ngono. Ni kusimama na utu na uhuru wa mawazo," imesema sehemu ya taarifa hiyo ya ACT.

Sakata hilo lilianza Novemba 28 mara baada ya Rais Dkt John Magufuli kufungua maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, ambapo kwa mujibu wa maelezo yake, mhadhiri huyo alibeba bango lililokuwa na ujumbe wa kumtaka Rais Magufuli aliangalie suala la kukithiri kwa rushwa ya ngono chuoni hapo lakini alizuiliwa.

Taarifa zinazosambaa leo, Kamati ya Maadili ya chuo hicho imemuita mhadhiri huyo katika kikao chake saa tisa mchana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post