AJALI YA GARI KUGONGA LORI YAUA WATU SITA PWANI

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

Watu sita akiwemo mtoto mchanga wa jinsia ya kike wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji cha Msata, barabara kuu ya Segera/Chalinze mkoani Pwani. 


Akithibitisha, kamanda wa polisi mkoani Pwani Naibu Kamishna wa Polisi ACP Wankyo Nyigesa alisema kwamba ajali hiyo imetokea Novemba 5, 2018 majira ya saa moja usiku baada ya gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster ikitokea Mkata kwenda Mbezi -Dar es salaam kuligonga kwa nyuma lori namba KBV 746C/ZE2861 FAW iliyokuwa imeegeshwa barabarani kutokana na kuharibika.

Amesema dereva wa Toyota coaster iliyosababisha ajali ambae hajafahamika jina lake alikimbia baada ya kutokea ajali.

ACP Wankyo alieleza kuwa waliopoteza maisha ni wanaume watano wenye umri kati ya miaka 30-40 ambao majina yao bado kufahamika. Alisema ,watu saba walipata majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mwili yao .

"Waliopata majeraha ni pamoja na wanaume wanne na wanawake watatu ambao wote wamepelekwa zahanati ya jeshi Kihangaiko -RTS na kituo cha afya Lugoba kwa matibabu zaidi "alisema Wankyo, akiongeza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa hospital ya wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi wa daktari.

Alitaja chanzo cha ajali, ni uzembe wa dereva wa gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster kujaribu kulipita bila tahadhari gari jingine lililokuwa limeegeshwa baada ya kuharibika na wanaendelea kumsaka.

Kamanda huyo alitoa rai kwa madereva kutii sheria za usalama barabarani na kuacha tabia za kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi ili kuepukana na ajali zembe. 

Wankyo aliwapa salamu madereva hao, kuwa hawatakuwa na muhali nao kwani watakamatwa na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم