Moja kati ya lori la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yanayotumika kusafirisha korosho mkoani Mtwara nchini Tanzania limepinduka likiwa na tani 15 za zao hilo.
Habari zilizoifikia MCL Digital zinaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyotokea juzi Jumanne Novemba 20, 2018 ni kufeli kwa breki za lori hilo.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 22, 2018 mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema hakuna askari aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa vibaya.
“Hizi ni baadhi ya changamoto tunazoendelea kukabiliana nazo na bahati njema ni kwamba askari wote wapo katika hali nzuri,” amesema Byakanwa.
Amebainisha kuwa kutokana na ajali hiyo korosho zote zilitawanyika barabarani.
Lori hilo lilipata ajali likiwa linatoka Wilaya ya Tandahimba kuelekea Manispaa ya Mtwara.
Novemba 12, 2018 Rais John Magufuli alisema Serikali ya Tanzania itanunua korosho zote za wakulima zilizolimwa mwaka huu 2018 na itachukua dhamana ya kuzitafutia soko.
Alitangaza uamuzi huo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri na manaibu waziri walioteuliwa Jumamosi ya Novemba 10, 2018.
Alisema JWTZ ndio watakuwa na jukumu la kusimamia kuhakikisha ulinzi kwenye maghala, korosho zinapimwa na wakulima wanalipwa.
Via Mwananchi
Social Plugin