Mshindi wa mashindano ya mbio za baiskeli yaliyopewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge, Masunga Duba akishangilia kuibuka mshindi na kujinyakulia Sh milioni 1.2, wa pili Gerald Konda (sh 900,000) na watatu Mungu Ataleta (Sh 500,000).
Meneja Uboreshaji Tija kutoka ACACIA, Janet Reuben akizungumza katika mashindano mbio za baiskeli yaliyopewa jina la Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge. Jumla ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa mashindano mbio za baiskeli yaliyopewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge wakiwakata upepo katika mashindano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza. Jumla ya washiriki 211 wametimua mbio katika mashindano hayo.
Baadhi ya washiriki wa mashindano mbio za baiskeli yaliyopewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge wakiwakata upepo katika mashindano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza. Jumla ya washiriki 211 wametimua mbio katika mashindano hayo.
Baadhi ya washiriki wa mashindano wakikata utepe kuanza mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza. Jumla ya washiriki 211 wametimua mbio katika mashindano hayo.
Baadhi ya washiriki wa mashindano wakianza kutimua mbio katika mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza. Jumla ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika mashindano hayo kwa lengo la kusaidia huduma za elimu kwa jamii zinazozunguka migodi ya Acacia.
NA MWANDISHI WETU
ZAIDI ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika kilele cha mashindano ya baiskeli ya ACACIA Imara Pamoja Cycle Challenge, ambayo lengo kuu ni kuchangisha fedha kutekeleza miradi itakayoboresha upatikanaji wa elimu kwa jamii zinazozunguka migodi kampuni Acacia kanda ya ziwa.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini –ACACIA kwa kushirikiana na Taasisi binafsi kutoka nchini Canada (CanEducate), yameshirikisha wanaume katika mbio za Kilomita 140 na wanawake km 87.
Mzunguko wa mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza ulianza na kumalizikia katika Hoteli ya Malaika Resort kwa kupitia maeneo ya Kibandani, Igombe, Sangabuye, Kayenze, Nyanguge na Usagara, Buhongwa.
Akizungumza katika kilele cha mashindano hayo, Meneja Uboreshaji tija wa kampuni hiyo, Janet Reuben alisema jumla ya washiriki 211 wameshiriki katika mbio hizo.
Alisema kila mwaka ACACIA imekua ikidhamini mashindano ya baiskeli ya kanda ya ziwa chini ya jina la Acacia Tufanikiwe Pamoja Cycle Challenge.
“Hata hivyo, mwaka huu mashindano hayo yamepewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge ili kuakisi dira mpya ya kampuni inayolenga kujenga mahusiano imara zaidi na jamii na wadau wetu. “Pia uamuzi huu wa kubadili jina unatokana na kuongezeka kwa kipengele cha uchangishaji fedha katika mashindano ya mwaka huu kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu.
“Kwa niaba ya uongozi wa Acacia kwa kupitia migodi yetu ya dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara, wadau wetu CanEducate na kamati ya maandalizi, nipende kuwashukuru kwa uwepo wenu leo, pia nawapongeza washindi na washiriki wote kwa kumaliza mbio hizi salama,” alisema.
Alisema uamuzi wa kuendelea kujihusisha na mbio za baiskeli umechangiwa na mapenzi makubwa ambayo watu wa kanda ya ziwa wanayo juu ya mchezo huo.
“Mpango huo pia unatoa kipaumbele katika kuhakikisha jamii zetu – hasa watoto wa kike - wanapata elimu bora kama njia moja wapo ya kujikwamua na umaskini na kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuinua uchumi na hali za maisha ya watanzania kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Acacia imeelekeza zaidi ya asilimia 38 ya bajeti yake ya kutelekeza miradi ya kijamii, katika miradi ya elimu. Baadhi ya miradi ya elimu ni pamoja na ujenzi wa madarasa, nyumba za waalimu, mabweni ya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike na ukarabati wa maktaba sita kwenye shule zinazozunguka migodi yetu,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika udhamini wa wanafunzi unaofanyika kati ya Acacia na CanEducate.
“Baadhi ya matumizi yaliyopangwa kwa ajili ya fedha hizo ni kama ifuatavyo; Fedha hizo zitasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zisizojiweza na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia sare na vifaa vingine vya shule ikiwemo vitabu na vifaa mbalimbali.
“Fedha hizo pia zitaelekezwa katika kusaidia wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaotoka kwenye maeneo yanayozunguka migodi yetu kwa kuwalipia ada za mitihani, gharama za malazi na usafiri,” alisema.
Aidha, Rais wa Chama Waendesha Baiskeli nchini, Godfrey Mhagama alimtangaza mshindi wa kwanza katika mbio hizo kwa upande wa wanaume kuwa ni Masunga Duba aliyejinyakulia Sh milioni 1.2, wapili Gerald Konnda (sh 900,000) na watatu Mungu Ataleta (Sh 500,000).
“Kwa upande wa wanawake mshindi ni Laurencia Luzuba (Sh milioni moja) na wa pili Tatu Malulu (Sh 800,000),” alisema.