Baada ya kuzungumza na Serikali, makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem amesema kuna masharti wamekubaliana kabla Tanzania haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani (Sh680.5 bilioni) kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Ghanem alisema benki hiyo inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote bila kujali hali zao, hivyo kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito au kingine chochote ni kwenda kinyume na mkakati wa elimu jumuishi.
“Wataalamu wetu watashirikiana na Serikali kuona ilivyojiandaa kutoa elimu kwa wasichana wote. Tutakapojiridhisha bodi ya wakurugenzi itaidhinisha mkopo husika. Kuchelewa kwake kutategemea lini Serikali itatekeleza masharti tuliyokubaliana,” alisema.
Mkopo huo ilikuwa ujadiliwe na kuidhinishwa Oktoba 30, lakini kutokana na msimamo wa Serikali kutotoa fursa ya kuendelea na masomo wasichana wanaopata mimba, bodi ya benki hiyo ilisitisha kuujadili. Kwa utaratibu wa benki hiyo, kabla mradi wowote haujaidhinishiwa fedha zinazohitajika, huujadili kwanza. “Mradi wa Tanzania haujajadiliwa. Lakini kwa mazungumzo tuliyofanya, utajadiliwa Serikali itakapotimiza masharti tuliyokubaliana,” alisema Dk Ghanem.
Baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, Rais John Magufuli alisema benki imekubali kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.
“Kwa hiyo, (Dk Hafez) amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha,” alisema Rais Magufuli.
Vilevile, Dk Ghanem alisema walizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Takwimu na wameishauri Serikali kuhakikisha wadau wake wanakuwa huru kukusanya na kutumia takwimu.
Alisema WB haiwezi kufanyakazi bila takwimu ambazo zitakusanywa kwa uhuru, lakini masharti yaliyomo kwenye muswada, huenda yakazorotesha ufanisi wake.
Mabadiliko ya Muswada wa Takwimu yaliyofanyika mwaka huu na kuridhiwa na Bunge, yanazuia mtu au taasisi yoyote kukusanya, kutafsiri au kutumia takwimu lazima zithibitishwe na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Social Plugin