Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka kampuni ya Nyati Resources inayofanya shughuli za uchimbaji dhahabu katika Kijiji cha Ngula wilayani Geita, kusitisha mara
moja kutoa gawio la umiliki wa ardhi kwa serikali ya Kijiji hicho baada ya mjane mmoja kulalamika kunyang’anywa ardhi hiyo kwa madai kuwa ndiye mmiliki halali.
Biteko ametoa zuio hilo Novemba 02, 2018 baada ya kufanya ziara katika mgodi wa Ngula kukagua shughuli za uchimbaji madini, kusikiliza na kutatua kero zinazohusiana na sekta
ya madini pamoja na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika mgodi huo.
Akisikiliza mgogoro wa umiliki wa ardhi katika mgodi huo, mjane huyo Bi. Mindi Masasi anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 80 alieleza kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo tangu mwaka 1954, na kwamba kampuni ya Nyati Resources ilipoanza shughuli zake mwaka jana ilikuwa ikimlipa gawio la umiliki wa ardhi lakini mwezi Aprili mwaka huu serikali ya Kijiji cha Ngula kupitia Mwenyekiti wake Symphorian
Mchael ilidai kumiliki ardhi hiyo na hivyo kuanza kupokea gawio kutoka kwa kampuni hiyo.
Kufuatia malalamiko hayo, Biteko alimwagiza Christopher Nilla ambaye ni Meneja wa kampuni ya Nyati Resources kusitisha utoaji wa gawio hilo hadi pale tume huru ya uchunguzi itakapoundwa na kutoa majibu sahihi nani mmiliki wa ardhi hiyo inayokadiriwa kufikia heka 350.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngulla, Symphorian Mchael kuchukua maamuzi ya kuweka zuio kwa kampuni ya Nyati Resources kutoa gawio kwa Bi. Mindi Masasi anayedai
kumiliki eneo hilo baada ya vikao vyote vya kutafuta mmiliki halali kukaa na kubaini kwamba eneo hilo ni la Serikali ya Kijiji.
Na George Binagi-GB Pazzo
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (kushoto), akimsikiliza mjane Bi. Mindi Masasi (kulia) anayedai kuwa mmiliki halali wa eneo la mgodi wa Ngula uliopo katika Kijiji cha Ngula wilayani Geita. Eneo hilo limechukuliwa na Serikali ya Kijiji cha Ngula na hivyo kuibua mgogoro baina ya bibi huyu na serikali ya Kijiji.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (kushoto), akimsikiliza Habi Makanika (kulia) ambaye ni kijana wa Bi.Mindi Masasi (katikati) wakati akisikiliza mgogoro wa umiliki wa ardhi baina ya bibi huyo na serikali ya Kijiji cha Ngula wilayani Geita.
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (kushoto), akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Ngula wilayani Geita.
Mwenyekiti Kijiji cha Ngula, Symphorian Mchael (kushoto), Mjane Bi.Mindi Masasi anayedai kuwa mmiliki halali wa eneo la mgodi wa Ngula (katikati) pamoja na Diwani Kata ya Bujula (kulia), wakisikiliza maamuzi ya Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (hayupo pichani) baada ya kusikiliza mgogoro wa umiliki wa eneo la mgodi wa Ngula.
Baadhi ya wachimbaji wadogo katika machimbo ya Ngula wilayani Geita, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko (hayupo pichani).
Tazama Video hapa chini