Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya amesema hamahama ya ya wabunge na madiwani wa upinzani kwenda Chama cha Mapinduzi (CCM) wengi wao wanafuata maslahi binafsi na sio kumuunga mkono Rais John Magufuli.
Kauli hiyo ya Kambaya imekuja siku moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF Abdallah Mtolea kujiuzulu ubunge na nafasi zote za uongozi alizokuwa nazo ndani ya chama hicho jana Alhamis Novemba 15, bungeni jijini Dodoma na kutangaza kujiunga na CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya CUF leo Ijumaa Novemba 16, Kambaya amesema chama hicho hakina mpango wala hakijaitisha kamati ya maadili na nidhamu ili kumjadili mwanachama yoyote si wiki ijayo wala mwezi ujao hivyo Mtolea aliamua kwa utashi wake mwenyewe kuhama na sio kwamba amesikia anataka kufukuzwa.
“Kuwa na mgogoro na chama hakuwezi kufanya uache ubunge kwasababu unapochaguliwa unaenda kufanya kazi ya wananchi na si chama, hivyo Mtolea kahama mwenyewe asisingizie alikosa ushirikiano.
“Wengi wao wanaohamia CCM wanautaka ‘uWaitara’ kwa maana kuwa wanataka kuchaguliwa kushika nyadhifa serikalini kama kuteuliwa kuwaWaziri au Naibu Waziri kama alivyoteuliwa mbunge wa Ukonga Mwita Waitara kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, “ amesema Kambaya.
Social Plugin