Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Breaking : ABDALLAH MTOLEA AJIUZULU UBUNGE NA NYADHIFA ZOTE CUF



Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), ametangaza kujivua unachama wa chama chake na kujiuzulu ubunge, akitaja sababu kuwa ni mgogoro kati ya wanachama wanaomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho na wale wanaomtambua Maalimu Seif Shariffu Hamad, kuwa Katibu Mkuu.

Tofauti na wabunge wengine, Mtolea alitangaza uamuzi wake ndani ya ukumbi wa Bunge wakati wabunge wakijadili Muswada wa Sheria Ndogo ya Fedha wa mwaka 2018.

“Sijui mnaoshangilia mnashangilia nini, lakini tulio ndani ndiyo tunaujua huu mgogoro, imefikia hadi hatua ya kutishiana maisha huko mitaani,” amesema Mtolea.

“Kwa hiyo nawashukuru wote kuanzia wewe Spika (Job Ndugai) kwa ushirikiano tuliokuwa nao hapa, Waziri Mkuu, wabunge wenzangu haswa wa kambi ya upinzani ambao mmekuwa karibu na mimi hata wale ambao hawatafurahishwa na uamuzi wangu huu.

“Najiuzulu nikiwa bado natamani kuwahudumia wananchi wa Temeke kwa hiyo nawakaribisha vyama vyote kuanzia Chadema, NCCR na CCM kujadiliana namna tutakavyoweza kushirikiana,” amesema.

Mtolea pia alitoa shukrani kwa wanachama wote wa CUF ambao hawamuungi mkono Profesa Lipumba.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Spika alimtaka kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ambapo Mtolea alitii amri hiyo na kumpa mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira Kazi na Vijana, Jenister Mhagama, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini huku Mbunge wa Tunduma (Chadema), Pascal Haonga akikataa kupewa mkono.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com