Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya Meryprisca Mahundi (katikati) akimkisikiliza kwa makini Afisa Mtendaji Kata ya Sangambi kijiji cha Igundu Joseph Nangale ,kuhusiana na namna ambavyo wafugaji wamefanya uhalibifu wa vyanzo vya maji katika kjiji hicho.Picha David Nyembe
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya Meryprisca Mahundi akiwa katika harakati za kujionea maeneo ya vyanzo vya maji ambayo yamehalibiwa vibaya na baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Igundu kutokana na kunywesha mifugo katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh Meryprisca Mahundi (Katikati)akiteta jambo na viongozi wa vijiji vinavyo zunguka kata ya Sangambi ambako kumefanyika uhalibifu wa vyanzo vya maji kutokana na baadhi ya wafugaji wa vijiji hivyo kunywesha mifugo yao sanjali na kupitisha mifugo katika maeneo ya vyanzo hivyo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh Meryprisca Mahundi akizungumza na wananchi wa Kata ya Sangambi (hawapo pichani) mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea maeneo ya vyanzo vya maji ambako kumefanyika uhalibifu mkubwa kutokana na baadhi ya wafugaji kupitisha mifugo yao.
Wananchi wa kijiji cha Igundu wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chunya Merryprisca Mahundi (hayupo pichani) mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea maeneo ya vyanzo vya maji ambako kumefanyika uhalibifu
mkubwa kutokana na baadhi ya wafugaji kupitisha mifugo yao.
Na David Nyembe, Chunya
MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Maryprisca Mahundi, amewapa wiki tatu wafugaji wa Kijiji cha Igundu katika Kata ya Sangambi wilayani humo kuhamisha mifugo yao na kuipeleka katika Kijiji cha Paris ambacho kimetengwa kwa ajili ya wafugaji.
Ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika kijijini hapo ambapo alisema lengo la kuondoa mifugo hiyo ni kumaliza mgogoro kati ya wakulima wa kijiji hicho na wafugaji pamoja na kuokoa chanzo cha maji ambacho wakazi wa eneo hilo wanakitegemea.
Alimuagiza Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Joseph Nangale, kusimamia na kuhakikisha mifugo hiyo inahamishwa huku akimtaka kutumia nguvu iliyotumika kuwazuia wakulima kufanya shughuli zao karibu na chanzo cha maji.
Mahundi alisema amechoshwa na migogoro ya wakulima na wafugaji katika kijji hicho cha Igundu na kwamba agizo lake hilo ni la mwisho na kwamba atakaporudi tena kwenye kijiji hicho na kukuta inaendelea hakutakuwa na majadiliano tena na kwamba wasije wakamlaumu.
“Mkae chini mjadiliane na mkubaliane idadi ya mifugo ambayo kila mfugaji wa kijiji hiki atatakiwa kubaki nayo hapa, nimewapa siku 10 viongozi wenu waniletee taarifa ya majidiriano hayo, lakini nimewashauri kila mfugaji abaki na mifugo 10,” alisema Mahundi.
Alisema idadi hiyo aliyopendekeza kila mfugaji abaki nayo kijijini hapo ni rahisi kuimudu ili isiingie kwenye mazao ya wakulima na kwamba itasaidia kumaliza migogoro.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Nangale alikiri kijiji hocho kuwa na idadi kubwa ya mifugo kuliko uwezo wa eneo la kijiji hicho hali ambayo inapelekea migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.
Alisema migogoro hiyo ilikuwa inaibuka baada ya mifugo kuwashinda wafugaji na kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na hivyo kuwafanya wakulima waanze kutaka kulipiza kisasi.
Aliahidi kushiriiana na halmashauri nzima ya kijiji hicho katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya la kuondoa mifugo na kwamba watayashirikisha makundi yote ili kufikia mwafaka ambao hautaleta shida.
“Kijiji cha paris kina eneo kubwa kwa ajili ya mifugo na ni eneo rafiki kwa sababu hakuna mwingiliano na shughuli zingine za kibinadamu, tulikitenga maalumu kwa ajili ya wafugaji,” alisema Nangale.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya aliwatahadharisha viongozi wa vijiji wanaopokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili waingize mifugo kwenye vijiji vyao kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria endapo watabainika.