Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WA MBARALI MKOANI MBEYA WATINGA IKULU KUMUONA RAIS

Mwenyekiti anayewawakilisha wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Patrick Mnyota (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam juzi, kuhusu mgogoro wa ardhi dhidi ya mwekezaji wa Kampuni ya Highland Estates Limited. Kulia ni mkazi wa Mbarali, Job Gwimile. 


Na Dotto Mwaibale

WANANCHI wa Mbarali mkoani Mbeya wametinga Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuona Rais Dkt.John Pombe Magufuli ili awasaidie kupata mashamba yao yanayodaiwa kuchukuliwa na mwekezaji wa kampuni ya Highland Estates Limited.

Hatua ya kuja Ikulu kumuona Rais ilifikiwa baada ya viongozi wa mkoa huo kudaiwa kushindwa kutatua mgogoro huo kutokana na maslahi ya mmiliki wa kampuni hiyo ambaye ni Mbunge wa Mbarali.

Aliwataja wakuu wa mkoa huo ambao walishindwa kuutatua mgogoro huo kuwa ni Abbas Kandoro (ambaye kwa sasa ni marehemu), Amosi Makala na wa sasa Mheshimiwa Albert Chalamila ambaye amedaiwa kuwatisha wananchi wanaofuatilia mgogoro huo kuwa atawakamata na kuwaweka ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti anayewawakilisha wananchi hao, Patrick Mnyota alisema wamehangaika sana na mgogoro huo lakini bado hawajapata mafanikio kutokana na baadhi ya viongozi kuwa upande wa mwekezaji.

"Tumerudi nyuma sana kiuchumi kwani maisha yetu yote kwa asilimia 100 tunategemea kilimo na ardhi ambayo tulikuwa tukiitegemea ndiyo hiyo imechukuliwa na mwekezaji huyo tunamuomba Rais wetu mpenzi wa wanyonge atusaidie jambo hili" alisema Mnyota.

Manyota alisema wananchi waliopo kwenye mgogoro huo ni kutoka vijiji vinavyozunguka mashamba mawili ya asili yaliyoanzishwa miaka ya 60 ambavyo ni Nyeregete, Urunda, Ibohora, Warumba, Imalilo (Songwe) na Mwakaganga kilichopo Ubaruku.

Alisema jumla ya ekari zilizopo katika mgogoro huo ni 3,207.63 hivyo kuathiri familia nyingi kwa kukosa chakula na mzunguko wa kiuchumi kuwa duni ukizingatia kuwa katika kipindi cha miaka 45 wamekuwa wakiyatumia mashamba hayo kwa kilimo.

Alisema wananchi wanauliza kwanini mgogoro huo hutokee hivi sasa kipindi cha mbunge huyu mbona katika kipindi cha Mbunge Edmund Mjengwa aliyeongoza jimbo hilo kwa miaka 15, Estelia Kilasi miaka 10 na Modestus Kilufi miaka mitano mgogoro huo haukuwepo.

"Kama kweli mashamba hayo yapo katika ramani ya shamba la NAFCO ya miaka 70 tunamuomba Rais Dkt. John Magufuli atusaidie kutatua mgogoro huu dhidi ya mwkezaji huyo kwani mashamba hayo tumekuwa tukiyaendeleza kwa miaka yote tangu uhuru" alisema Mnyota.

Alisema suala hilo lilifika hadi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi lakini bado halijapatiwa ufumbuzi ingawa katika migogoro mingine ya aina hiyo amekuwa akiwasaidia wananchi ikiwemo pamoja na kufuta umiliki wa ardhi na kuwapatia wananchi.

Mnyota amedai kuwa hivi sasa mwekezaji huyo amekuja na ramani mpya ya shamba ambayo imetayarishwa mwaka 1987 na kufanya shamba hilo kuwa  na ramani zaidi ya moja ambapo wananchi wa eneo hilo wanaitambua ramani halisi ya shamba ni ile ya mwaka 1970.

Alisema hata hivyo kama ramani hiyo inaonesha mpaka wa shamba ni huku tunakoishi na kulima (hizi ekari 3,207.63) wanaiomba serikali iwaachie waendelee kumiliki kutokana kuwa shughuli zao za uzalishaji katika maeneo hayo ndio maendeleo yao kielimu, afya, makazi na kiuchumi.

Alisema shamba la Mbarali Estates Limited ni mwiba sana kwa wananchi wanyonge kwani hakuna kiongozi yeyote mkoani humo anayewasikiliza imefikia hatua mwekezaji huyo anatumia jeshi la polisi kufukia mifereji ambayo inategemewa kwa umwagiliaji wa mashamba yao na ile iliyokuwa ikitoa maji kwa wananchi kwa kazi za kilimo toka shirikani imefungwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com