RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amefunga mjadala kuhusu mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, akisema kuwa hategemei kutenga fedha kwa ajili ya mchakato huo kwa sasa. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).
Akizungumza katika kongamano kuhusu hali ya uchumi na siasa nchini lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jijini Dar es Salaam,leo Novemba 1,2018 Rais Magufuli amesema kuliko fedha kutumika katika mchakato huo, ni bora zielekezwe katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli.
Aidha, amesema kama kuna watu wanataka kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya mchakato huo, ni bora wasaidie katika ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge-SDG).
“Tusitumie hela ya kupeleka watu bungeni wakalipane posho za kila siku, tunataka hizo fedha zitumike kujenga reli, SDG, kuimarika kilimo, na ndio maana kuna mataifa makubwa katiba zao zimeundwa miaka kadhaa zilizopita. Tutakaa kubishana kupoteza pesa ‘for nothing’, huu si wakati wake,”amesema na kuongeza Rais Magufuli.
“Sitegemei kupanga hela kwa ajili ya watu kula kwa sasa hivi, na kama wako watu wanataka kutusaidia hizo fedha, watusaidie kujenga reli na SDG. lakini sikatai kusikiliza maoni ya watu, kuna ushauri tunapokea, Lakini ninachotaka kuwambia tunaenda vizuri.”
Chanzo- Mwanahalisionline