RAIS John Mafuguli amesimulia alivyofunga ndoa na mke wake Janeth bila shamrashamra wala mbwembwe kama ilivyozoeleka.
Akizungumza katika Kongamano la Siasa na Uchumi lililofanyika jana jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema siku hiyo hakuvaa suti wala mke wake hakuvaa gauni la harusi.
Alisema siku hiyo alivaa suruali na shati la kawaida na hata pete aliyomvalisha mke wake Janeth alinunuliwa na Padri wa Kanisa la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo ilikuwa ya madini ya shaba.
“Nimefurahi kupata mwaliko wa kuja hapa, Chuo Kikuu ambacho nina historia nacho. Nimesomea hapa shahada yangu ya kwanza na nilikuwa nakaa bweni namba tatu baadaye nilikaa bweni namba moja jengo F,” alisema Rais Magufuli.
Alisema jambo kubwa analokumbuka ni pale alipofunga ndoa katika Kanisa la Chuo Kikuu na Padri Msemwa ambaye kwa sasa yuko mkoani Tanga ndiye aliyewafungisha.
“Kikubwa Chuo Kikuu nilifungia ndoa hapa na utofauti na ndoa mlizozizoea mimi sikuvaa suti na wala mke wangu hakuvaa shela, lakini tulifunga ndoa kwenye Kanisa la Chuo Kikuu. Tulikwenda kwa Padri nakumbuka siku hiyo pete alitununulia yeye na ilikuwa ya shaba na alitupa soda. Mimi nilikunywa Pepsi na mke wangu alikunywa Mirinda,” alisema.
“Si kwamba sikuwa na uwezo ila nilijua huo ndio utaratibu na kuanzia hapo hata watoto wangu watatu wamefunga ndoa nikiwa Rais na hamjawahi kusikia sherehe zao mpaka leo,” alisema.
Kwenye hotuba yake, Rais Magufuli alizungumzia mafanikio ya serikali yake yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu, tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015.
“Uongozi ni mgumu, ukiingia chumbani kwangu hata leo utakuta mafaili yamejaa hadi mlangoni, hata wakati mwingine huwa najiuliza watangulizi wangu walikuwa wanafanyaje? Na kila faili lina umuhimu na huwezi kumpelekea mtu mwingine, kazi ya urais ni ngumu na inahitaji moyo,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ni mengi na kila mwezi serikali imekuwa ikipeleka Sh. bilioni 23 kwa shule nchini kuendeleza sera ya elimu bure na kwamba fedha hizo zinapelekwa moja kwa moja katika shule bila kupitia halmashauri.
Pia alisema serikali imeongeza bajeti katika mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia Sh. bilioni 483.
Rais Magufuli alisema zaidi ya Sh. bilioni 660 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara za Jiji la Dar es Salaam, kupanua uwanja wa ndege namba tatu kwa kutenga Sh. bilioni 560.
Alisema wamepanga pia kununua rada zitakazofungwa katika maeneo yote ya nchi, ili ndege zitazokuwa zinapita katika anga ya Tanzania ziweze kulipia.
Chanzo - Nipashe