Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JWTZ YAKABIDHIWA RASMI KIWANDA CHA KUBANGUA KOROSHO BUKO

Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) leo limekabidhiwa rasmi kiwanda cha kubangua korosho cha Buko kilichopo mkoani Lindi tayari kwa kuanza kupokea na kubangua korosho.


Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku mbili baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli kutangaza kwamba Serikali itanunua korosho za wakulima.


Makabidhiano hayo yamefanyika kati ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na Kanali Rajabu Mabele na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo pamoja na mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Adam Kamana.


Akizungumza baada ya kukabidhiwa kiwanda hicho, Kanali Mabele amesema wanaanza na tathmini kabla ya kuingia kwenye kazi rasmi.


“Tunafanya tathmini, nia yetu ni kukiboresha katika kiwango cha juu ili kuweza kutekeleza maelekezo ambayo ametoa mheshimiwa Rais ili kwenda na mwendo ambao anautaka yeye,” alisema Kanali Mabele.


Kuhusu ulinzi wa maghala ya korosho amesema ulishaanza kufanyika na ulifanywa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kama alivyoagiza Rais John Magufuli.


“Tumefika pale kusaidiana na vyombo ambavyo vipo katika ulinzi wa maghala yote ambayo yako mkoa wa Lindi pamoja na mikoa mingine ambayo imetajwa,” alisema Kanali Mabele


Naye mwakilishi wa TADB, Adam Kamana amesema wakulima wamekuwa wakinyanyasika kwa muda mrefu na hata Serikali inapoweka viwanda vinakufa ili zao hilo lisafirishwe kwenda nje bila kubanguliwa.


“Katika mnyororo mzima wa mazao lazima tujifunze kutouza malighafi kutoka shambani, sasa mheshimiwa Rais ameliona ametoa agizo, tuko hapa tumeshaanza kutembea, benki ya kilimo tunatembea na wakulima Tanzania nzima tumekuja kutii agizao.”


Kuhusu suala la malipo amesema fedha tayari ipo na ana uhakika wakulima wataanza kulipwa kesho Alhamisi kwani rais amewatuma kununua korosho kwa bei ya Sh 3,300 kwa kilo.


“Tumekuja kwa kusema ukweli pesa tuko nayo iko kwenye system zetu zote, ipo benki ya kilimo hapa ninavyoongea hata tukiongea baadaye kuna kikosi kazi kitakuwa kinafanya kazi baada ya muda huu ili kuangalia utaratibu upi tuufuate kuwalipa wakulima.’’

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com