Picha : MWANAMUZIKI KING KIKI ATOA NENO KWA MAOFISA WA POLISI CHUO CHA KURASINI DAR


Mwanamuziki Mkongwe nchini Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki' akizungumza na maofisa wa Jeshi la Polisi waliopo katika mafunzo Chuo cha Polisi cha Kurasini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuhusu haki za wanamuziki hapa nchini ambapo ameliomba jeshi la polisi kuendelea kusimamia sheria ya haki miliki za wanamuzi ili kazi zao zisiishie kwa maharamia. Mada katika mkutano huo zilitolewa na viongozi wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO)
Maofisa wa polisi wa chuo hicho wakisikiliza mada.
Katibu wa TAMUFO Stellah Joel Diana akizungumza na maofisa hao.
Rais wa TAMUFO Dkt. Donald Kisanga akizungumza na makamanda hao.
Maofisa hao wakiandika dondoo mbalimbali katika mkutano huo.

Mshauri wa masuala ya kisheria wa TAMUFO, Mkaguzi wa Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo akitoa mada katika mafunzo hayo. 
Mkutano ukiendelea.
Makamanda wakiwapashia makofi viongozi hao wa TAMUFO kwa utoaji wa mada nzuri.
Mwanamuziki wa nyimbo za injili Emmanuel Mbasha akizungumza na makamanda hao.
Picha ya pamoja

Na Dotto Mwaibale

MWANAMUZIKI Mkongwe hapa nchini Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki' ameliomba jeshi la polisi kuendelea kusimamia sheria ya haki miliki za wanamuzi ili kazi za wanamuziki hao zisiishie kwa maharamia.

Ombi hilo alilitoa mwishoni mwa wiki wakati viongozi wa Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO), ukitoa mada kwa maofisa wa Jeshi la Polisi  waliopo katika mafunzo Chuo cha Polisi cha Kurasini jijini Dar es Salaam kuhusu haki za wanamuziki hapa nchini.

"Ninyi wenzetu jeshi la polisi ndio tunaowategemea katika kusimamia sheria hii tunaamini mtatusaidia kazi zetu zisiibwe na maharamia" alisema King Kiki.

Akizungumza na katika mafunzo hayo Rais wa TAMUFO, Dkt. Donald Kisanga alisema lengo la mafunzo hayo ya siku moja kwa maofisa hao ni kuwajengea  uelewa wa ulinzi wa kazi za muziki ikiwepo  kudhibiti na kuwakamata maharamia wa kazi muziki hapa nchini.

Katibu Mkuu wa TAMUFO Stellah alisema umoja huo ulishatoa mapendekezo kupitia waraka maalumu kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt Harisson Mwakyembe ili mtu yeyote atakayebainika akihujumu kazi za wasanii ashitakiwe kwa makosa ya jinai.

Alisema TAMUFO pia inaandaa mapendekezo ya kupeleka serikalini ya kuweka dawati la jinsia katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchini ambayo yatakuwa yakishughulikia wizi wa kazi za wanamuziki.

Mshauri wa masuala ya kisheria wa TAMUFO, Mkaguzi wa Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo akitoa mada katika mafunzo hayo yaliyowahusisha maofisa wa polisi zaidi 500 kutoka mikoa yote ya Tanzania alisema ni muhimu kwa maofisa hao kujua sheria hizo kwa kuwa wao ndio wanaozisimamia.

"Changamoto kubwa tuliyonayo ni maofisa wetu wa polisi kutojua sheria zinazosimamia kazi za wasanii wetu ndio maana tumeona tuwapige msasa ili waijue na kuweza kuongeza nguvu ya kuwakamata maharamia wa kazi hizo za wanamuziki" alisema Kyogo.


Alisema sheria ya mtandao ya mwaka 2015 sheria namba 14 mtu yeyote atakaye bainika akidurufu nyimbo na kumpa mtu mwingine bila ya ruhusa ya mmiliki wa wimbo husika adhabu yake ni kifungo kisicho zidi miaka mitatu au kulipa faini shilingi milioni tano.

Aliongeza kuwa kwa mtu atakayebainika akidurufu nyimbo za wasanii kwa lengo ya kuziuza kifungo chake ni miaka mitatu au kulipa faini shilingini milioni 20 hivyo alitoa rai kwa wananchi kuacha kuchezea kazi za wasanii kwani sheria hizo zipo na zinafanya kazi.

Alisema kazi za wasanii zikilindwa zitawanufaisha kwa kuziuza na zitatoa ajira hivyo ni muhimu jamii ijengewe uelewa ili waache kuiba kazi hizo ambazo zikilindwa vizuri zitaweza kutangaza utamaduni wetu na serikali itapata mapato kutokana na kodi watakazolipa wahusika baada ya kuziuza.

Maofisa hao wa polisi waliitaka TAMUFO ijihimarishe zaidi katika kazi yao hasa kwa kusimamia mapato yote ya wanamuziki kama inavyofanyika katika nchi zingine jambo likatalosaidia kuyalinda maslahi ya wanamuziki badala ya kuwategemea polisi ambao wanamajukumu mengi ya kesi za jinai.

"Tunawaomba TAMUFO mjiongeze wekeni utaratibu wa nyinyi kuwa wakusanyaji wa mapato ya wanamuziki jambo ili litasaidia wanamuziki kupunguza uharamia na pia litatupungizia kazi hata sisi wasimamizi wa sheria" alisema mmoja wa maofisa hao wakati akiuliza maswali.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post