Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA KIVULINI LAZINDUA KAMPENI KUTOKOMEZA UKATILI SHINYANGA



Shirika lisilo la serikali Kivulini la Mkoani Mwanza limezindua kampeni mahsusi ya wilaya ya Shinyanga kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,ndoa na mimba za mapema ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa kike waliopo kwenye hatari ya kupata ujauzito wa mapema unaosababisha kushindwa kufikia ndoto zao.
Katika kampeni hiyo ambayo imezinduliwa leo jumatano Novemba 14,katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ambapo mgeni rasmi katika uzinduzi huo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amesema serikali haitamfumbia macho mtu yeyote ambaye atakuwa na viashiria vya kufanya ukatili wa aina yoyote na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha matukio hayo yamekoma kwa kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaobainika kujihusisha na ukatili. 

“Niseme tu kama serikali hatuwezi kufumbia macho masuala haya,lazima tuyaongee na jamii ijue lakini pia ichukue hatua ya kutokomeza kabisa masuala haya ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,kwani kundi hili ni kubwa sana katika taifa letu,tunasikia malalamiko mengi sana yameelekezwa kwa kinababa,sitaki kusikia katika wilaya ya Shinyanga mambo hayo yakiendelea.”Alisema Mboneko. 



“Wazazi wote tunatakiwa tuwe na jukumu la kuangalia mienendo ya elimu kwa watoto wenu,tusiache wapotee njiani tutakukamata wewe mzazi mpaka mtoto atakapofanikisha azma yake ya masomo.”Aliongeza Mboneko 

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Yasini Ally amesema lengo la kampeni hiyo itafanikiwa endapo jamii itaipokea kwa maono chanya elimu ya ulinzi wa mototo,na kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwamba tayari shirika hilo limeunda vikosi vya mabadiliko ya kitabia katika wilaya ya Shinyanga na Kishapu ambavyo vimekuwa na matokeo mazuri katika mabadiliko ya kitabia. 

“Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayotajwa kuwa na vitendo vya ukatili,mimba na ndoa za utotoni hivyo tumeamua kuanzisha vikundi vya wana mabadiliko, wilaya ya Shinyanga tuna wanamabadiliko 100 na kishapu wanamabadiliko 200 ambao wamepewa mafunzo na kutoa elimu ya kutokomeza ukatili ,nyumba kwa nyumba,vitongoji,mashuleni,nyumba za ibada na kwenye mikutano ya hadhara.”Alisema Yasini 

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba amesema kampeni hiyo itasaidia kupunguza kama sio kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwani tatizo hilo limetajwa kuwa kubwa katika halmashauri hiyo na kuiomba jamii kutoa ushirikiano katika mapambano hayo. 

“Nawaomba wana Didia na wana halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tushirikiane kwa pamoja,tuanzie kwenye ngazi ya familia hadi kwenye ngazi ya taifa ili kuwa na taifa lililoendelea kwani changamoto kubwa katika mapambano haya ni jamii kukosa ushirikiano." Alisema  Mahiba.

“ Ukiangalia takwimu ukatili wa kijinsia kuanzia mwezi Januari hadi mwezi novemba mwaka huu katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa upande wa ubakaji wa watoto ni kesi zilizoripotiwa ni 25,vipigo kwa wanawake kesi 12 naamini kuna kundi kubwa linalofanyiwa vitendo hivyo lakini hawapo tayari kutoa taarifa.” aliongeza Mahiba. 

Mpango huo wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto,mimba na ndoa za utotoni unatekelezwa katika wilaya ya Shinyanga na Kishapu ukitekelezwa na shirika la Kivulini la mkoani Mwanza kwa kufadhiliwa na shirika la kimataifa Oxfarm. 
TAZAMA PICHA HAPA CHINI


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akisisitiza ushirikiano,katika kampeni hiyo.
 Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Kivulini Yasini Ally wakati akieleza ukubwa wa tatizo la vitendo vya ukatili kwa mgeni rasmi

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba akieleza namna halmashauri inavyopambana na vitendo vya ukatili,mimba na ndoa za mapema
 Mwanafunzi wa shule ya sekondari Don Bosco akieleza jinsi vyumba vya kupanga wanafunzi(Gheto) vinavyochangia mimba kwa wanafunzi wa kike.

 Mwanamabadiliko kutoka wilaya ya Kishapu akitoa shuhuda za namna alivyobadilika kuacha tabia za manyanyaso kwa mke na familia yake na kugeuka kuwa mfano bora. 
 Mwanafunzi wa Don Bosco akitoa maoni yake kuhusu njia mbalimbali za kujikinga kuepukana na mimba za mapema.
 Mwanakijiji wa Didia akieleza kinaga ubaga kuhusu wanaume kukimbia miji yao wakati wa mavuno na kujivinjari mijini.
 Kikundi cha ngoma kikiburudisha na nyoka
 Viongozi wa dini kata ya Didia
 Wanafunzi wa shule ya sekondari Dn Bosco wakiangalia michezo inayoendelea
 Kwaya ya Didia ikitoa jumbe kwa njia ya wimbo
 Wanamabadiliko kutoka wilaya ya Kishapu na Shinyanga

Wazazi wakati wa uzinduzi wa kampeni.

PICHA ZOTE NA MALAKI PHILIPO - MALUNDE1 BLOG.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com