Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara, wameanza kuziuza mbele ya Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, kwa bei ya juu ya Sh 3,016 huku bei ya chini ikiwa ni Sh 3,000 na kampuni 11 zilijitokeza kuomba kuzinunua.
Awali wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara walikataa kuuza korosho zao baada ya wanunuzi kuja na bei waliyoikataa ya Sh 2,717 hadi Sh 2,011 kwa kilo hatua iliyosababisha minada hiyo kusimamishwa hadi Rais Dk. John Magufuli alipotoa tamko la bei elekezi ya Sh 3,000.
Akizungumza wakati wa mnada huo, Tizeba, alisema wanunuzi wanapaswa kufuata maelekezo waliyopewa na Rais Magufuli na si vinginevyo ili kununua korosho hizo.
Alisema hatafurahishwa na kuona mnunuzi akiomba kununua korosho kwa bei isiyoridhisha itakayokuwa chini ya Sh 3,000 na hiyo itakuwa ni kinyume na makubaliano ya kikao cha wanunuzi.
“Nitashangaa kuona mnunuzi mwenye akili timamu akitoa barua na kutaka kuuziwa korosho chini ya shilingi 3,000 au akitaka kwa shilingi 2,500.
“Wafanyabiashara wasipangiwe muda wa kuchukua korosho ghalani kwa ajili ya usafirishaji na wasipangiwe kutumia bandari gani, wawe huru kulingana na maagizo yaliyotolewa na Magufuli,” alisema Tizeba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alisema wakulima wanapaswa kuwaepuka watu wanaofanya korosho kuwa jukwaa la siasa badala yake waangalie masilahi yao.
“Watu wanaotaka kukwamisha wakulima wasiuze tunapaswa kujua kuwa korosho inayotolewa hapa inauzwa kimataifa na wakati wowote sokoni bidhaa inaweza kupanda ama kushuka.
“Wapo wakulima walinunua korosho kinyume cha utaratibu hali inayowafanya wao watumie majukwaa ya siasa kuwarubuni nyinyi msiuze korosho, wapuuzeni na msiwape nafasi,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), Mohamed Mwinguku, alisema chama hicho kimeuza korosho tani 2,141 kwa bei ya Sh 3,016 hadi 3,000 kwa kilo huku tani 3,800 zikibaki ghalani.
“Awali tulikuwa na tani 7,000 ambazo zilikuwepo ghalani lakini kutokana na barua za tenda tulizosoma katika mnada tumelazimika kuuza tani 2,141 tu, jambo hili linatupa faraja kwa kuwa wanunuzi wameitikia wito wa Magufuli, tunaamini kuwa zilizopo na zitakazoongezeka zitauzwa mnada unaofuata,” alisema.