Abiria waliopaswa kusafiri kutoka manispaa ya Bukoba kwenda katika wilaya mbalimbali mkoani Kagera leo wameshindwa kusafiri, kutokana na madereva kugoma wakipinga kupandishiwa ushuru katika kituo kikuu cha mabasi.
Baadhi ya madereva wamesema hawakubaliani na hatua hiyo kwa sababu hakuna kilichoboreshwa katika kituo hicho ambacho hakina vyoo, nyumba ya kupumzikia abiria na kimejaa vumbi hali inayowasababishia adha kubwa hasa kipindi mvua zinaponyesha.
“Kama wanataka kupandisha ushuru basi waboreshe Stendi kwanza ili tuone mapato wanayokushanya kuwa yanafanya kazi” alisema Paskates Paschale.
Mafutah Rajab ambaye pia ni dereva alisema haifai wao kupandishiwa ushuru wakati nauli ya abiria bado ni ile ile tangu mwaka 2013, na kuwa mwaka huo walikuwa wakinunua mafuta kwa shilingi 1,750 lakini sasa wananunua kwa shilingi 2,600 kwa lita moja.
Naye William Wilbard alisema hawakushirikishwa katika mchakato mzima wa kupandisha ushuru, na kuwa wao wakiwa katika kituo hicho cha mabasi walisikia gari likipita linatangaza kuwa ushuru wa kuondoa gari katika kituo hicho umepanda.
Baadhi ya abiria waliokutwa wamekaa katika magari wakiwa na matumaini ya kusafiri waliomba serikali kuwasiliana na wadau wote wanaohusika na kukaa nao kikao ili kupata maamuzi ya pamoja, kuliko serikali kukaa na kuamua na matokeo yake wanaoumia ni abiria.
“Mimi naumwa, nilipaswa nisafiri kwenda Kyaka nikapumzike, lakini nimefika Stendi sijui kinachoendelea nikapanda gari lakini tangu nimepanda hadi sasa gari haliondoki, ndiyo nakuja kuambiwa kuna mgomo” alisema bibi Reocadia Petro.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kutetea Abiria Bashiru Samadu aliwataka wahusika wote kukaa meza moja na kupata muafaka maana wanaoumia ni abiria, ambao wamefika kituoni hapo wakiwa na matumaini ya kusafiri lakini wakakuta kuna mgomo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Richard Mihayo aliwataka madereva kuendelea kulipa kiwango kipya cha shilingi 2,000 kwa Hiace na shilingi 4,000 kwa Coaster kila wanapotoka katika kituo hicho, na kuwa uongozi wa manispaa utaendelea kufanyia kazi changamoto nyingine.
“Sheria hii ilipitishwa tangu mwaka 2005 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2008, inawezekana wengi wa wanaolalamika sasa wakati huo hawakuwepo, kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa sheria hii”, alisema Mihayo.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na madereva waliokuwa wakimsikiliza na hatimaye wakakubaliana kwenda kufanya mazungumzo na kupata muafaka kuhusiana na suala hilo.
Social Plugin