MAGUFULI : KAZI YA KUONGOZA NCHI NI NGUMU....NAHITAJI MAOMBI SANA KUTOKA KWENU


Rais John Magufuli amesema kazi ya kuongoza nchi ni nzito yenye kuhitaji umakini wa hali ya juu na akawaomba waumini wa dini zote na Watanzania kumuombea.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Novemba 4, 2018 wakati akitoa salamu zake kwenye maadhimisho ya miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

Amesema licha ya changamoto nyingi anazokutana nazo katika uongozi wake, haishi kujiuliza maswali viongozi waliopita walitumia mbinu gani kuhakikisha wanatatua yale waliyokumbana nayo.

“Nahitaji maombi sana kutoka kwenu na hata maoni, changamoto za kazi hizi ni ngumu sana nawaza hivi hawa wazee walionitangulia kina Mzee Kikwete (Jakaya), Mkapa (Benjamin) na Mwinyi (Ali Hassan) walimalizaje miaka 10, ni kazi nzito inahitaji maombi kwelikweli,” amesema.

Hata hivyo, amewapa moyo wananchi kuwa licha ya changamoto hizo ana imani kwamba nchi itafanikiwa
Rais Magufuli aliwaomba viongozi wa dini wahubiri amani, upendo na haki ili kujenga jamii iliyostaarabika na yenye kujua majukumu yake katika kuijenga nchi.

“Naamini wanaokula rushwa, wabakaji, mafisadi si wapagani tu wengine ni waumini wenu,” amesema.

“Tuwe na imani ya matendo na kuondokana na matendo yanayotutenganisha na Mungu tutaweza kuipeleka nchi mahali pazuri na kutimiza azma ya upendo.”

Kuhusu maadhimisho hayo, Rais Magufuli amesema anaamini kuwa miaka mingine 150 ya Jubilee hakuna ambaye atasherehekea, hivyo ni muda muafaka sasa kukumbuka waanzilishi wa kanisa hilo ili kuenzi juhudi zao.

“Katika kufikia mahali tulipo ambako sasa tunaweza kusherehekea, tuwakumbuke Wamisionari wa kwanza ambao walipambana na changamoto nyingi za kukatisha tamaa lakini hawakukata tamaa na hata wengine waliuawa.”

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kuijenga nchi yenye amani na upendo, kwani inatambua mchango wa madhehebu mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post