Jana Novemba 15, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya Chama cha CUF Abdalah Mtolea alijivua uanachama wa CUF na kujiuzuru Ubunge wa Jimbo la Temeke, huku akieleza chanzo kikiwa migogoro isiyoisha katika Chama cha CUF kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Tukio la kujivua uanachama wa CUF na kujiuzuru ubunge lilitokea ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati akichangia hoja katika mjadala uliokuwa unaendelea.
Ndugu Abdalah Mtolea jana hiyo hiyo alitangaza nia yake ya kuomba kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) akieleza msingi wa uamuzi huo ukiwa umejengwa katika ukweli kwamba wengi ya wapiga kura wake wamemshauri kujiunga na CCM.
Akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari, watumishi na baadhi ya wanachama wa CCM katika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma, Ndugu Mtolea alieleza sababu zinazopelekea kuomba kujiunga na CCM na kuwa amevutiwa na Mageuzi makubwa ya Kiuongozi na kazi nzuri inayofanywa na CCM na Serikali yake chini ya Ndugu John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikao hicho cha waandishi wa habari, watumishi na baadhi ya wanachama wa CCM kilihudhuriwa pia na Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM ambaye alimwelekeza kwenda katika tawi lililo karibu na makazi yake Wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam ili afuate utaratibu wa kuomba uanachama wa CCM.
Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
OFISI YA MAKAO MAKUU DODOMA
Social Plugin