Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Petter Msigwa amehoji juu ya tatizo la ajira nchini, na kuitaka serikali kuboresha vyuo vya ufundi ili wasihamasishe wanafunzi kwenda vyuo vikuu.
Mchungaji Msigwa amesema hayo katika Mkutano wa Bunge wa 13 katika kikao cha 7 alipokuwa akihoji swali kwenda kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira.
"Tatizo la ajira ni janga kubwa nchini kwetu, ni kwanini serikali isiimarishe vyuo vya veta ili vijana wetu wapate ujuzi utakaowafanya waweze kujiajiri, je serikali inaweza kutoa msisitizo kwa vyuo vya veta kuliko vyuo vikuu ambao wanaohitimu hawaajiriki," aliuliza Msigwa.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira amesema katika kufikia malengo hayo, serikali imeingia makubaliano na vyuo vya ufundi kwa kuwachukua wanafunzi waliohitimu wa kidato cha nne na la saba na kupatiwa mafunzo.
"Kama serikali tunatekeleza ujuzi kwa vijana wetu, tumeingia makubaliano na vyuo vya veta na Donbosco ili kutoa mafunzo ya ufundi mpaka sasa zaidi ya vijana elfu 8 tumewapatia mafunzo lakini malengo yetu ni kufikia vijana milioni 8." Amejibu Naibu Waziri Mavunde.
Social Plugin