Mgomo wa madereva wa magari ya abiria uliodumu kwa masaa kadhaa na kusababisha abiria kushindwa kusafiri kutoka manispaa ya Bukoba kwenda wilaya mbalimbali za mkoa wa Kagera umemalizika baada serikali ya wilaya na viongozi wa madereva kukaa meza moja ya mazungumzo na kufikia muafaka.
Jana madereva wa magari hayo walifanya mgomo wa kutoa magari yao katika kituo cha mabasi cha manispaa ya Bukoba wakipinga hatua ya kupandishiwa ushuru bila wao kushirikishwa.
Katibu tawala wilaya ya Bukoba Kadole Kilugala amesema katika kikao walichokaa na viongozi wa madereva na wadau wengine wa usafiri wamekubaliana masuala kadhaa ambayo madereva hao wanahitaji yafanyiwe kazi ikiwamo kituo hicho kuwekewa lami.
“Wanasema pia magari madogo yanayobeba abiria yaondolewe maana hayalipi kodi, vijengwe vyoo na miundombinu nyingine, kwa hiyo tumekubaliana waendelee na viwango vya zamani vya shilingi 1,000 kwa Hiace na shilingi 2,000 kwa Coaster, halafu tukutane tena Desemba 6 mwaka huu, ndipo tutaelezana masuala yapi yatatekelezwa na yapi hayatatekelezwa”, amesema.
Social Plugin