Waziri Jenista Mhagama ambaye yuko chini ya Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameitaja mikoa nane inayoongoza kwa kilimo cha bangi nchini.
Akiwa Bungeni akiwasilisha taarifa ya hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2017, Waziri Mhagama amesema mikoa inayoongoza kwa kilimo hicho ambacho kimepigwa marufuku nchini na ambacho ni kinyume na sheria, inaongozwa na mkoa wa Mara, Arusha, Njombe, Tanga, Simiyu, Rukwa, Geita na Morogoro.
Sambamba na hilo Waziri Jenista Mhagama amesema, licha ya mikoa hiyo kuwa vinara wa ulimaji bangi, kiasi cha bangi kilipungua kutoka tani 68.23 kwa mwaka 2016 na kufikia tani 52.19 kwa mwaka 2017, na ukamataji wa mirungi uliongezeka kutoka tani 21.6 kwa mwaka 2016 hadi kufikia tani 67.8 mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara tatu.
Hata hivyo Waziri Mhagama amesema mashamba ya mirungi ya ukubwa wa ekari 64.5 yaliteketezwa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Social Plugin