Ogechi Babalola alikuwa na furaha kama hiyo alipogundua kwamba alikuwa ameshika mimba na angejifungua kifungua mimba wake.
Lakini alipokwenda kuwafichulia dada zake, kila mmoja aligundua kwamba alikuwa anabeba mimba.
Watatu hao, waliozaliwa Nigeria ingawa kwa sasa wanaishi Marekani, walipigwa picha kwa pamoja, wakiwa wajawazito, picha ambazo zimewavutia watu si haba mtandaoni - wengi wakifurahia pamoja nao.
Kwanza Ongechi alikwenda kwa Chika Okafor na kumfichulia habari.
Onyeka Ufere, 30, alipofahamishwa, naye akawafahamisha kwamba naye alikuwa mjamzito.
Mmoja wao, Chika Okafor ndiye aliyepakia picha hizo kwenye mtandao wa Instagram na kuongeza ujumbe: "Kama wanifahamu vyema, basi wafahamu kwamba huwa nawapenda sana dada zangu. Nimekuwa nikigawana nao karibu kila kitu (mavazi, walimu, wazazi, chakula).
Sasa tutakuwa pamoja kwenye safari hii ya kusisimua ya kuwa mama. Mungu na wakati wake, ni kama mwujiza. Singefikiria hata wakati mmoja kwamba hili lingetokea."
Wameambia BBC kwamba hawakufahamu jinsi kisa chao kilivyokuwa cha kipekee.
Wote wameolewa, na wanatarajia kujifungua watoto wao wakiwa wameachana kwa wiki kadha tu.
"Kwangu na dadangu Chika, ulikuwa ni wakati wetu wa kwanza kushika mimba, na kwa hivyo wazo la kufanya hivi tukiwa peke yetu lilikuwa linatutia wasiwasi. Onyeka amepitia hili awali, ambapo alijaliwa watoto pacha," Babalola aliambia Yahoo Lifestyle.
Anasema hakuna kule kulalamika, kucheka na kusumbuka na kutokwa na machozi kwani katika kila analolipitia, anafahamu kwamba kuna mwenzake ambaye anapitia kitu sawa na hicho.
Babalola, 26, na Okafor, 27, wanatarajia kujifungua watoto wavulana.
Ufere, 30, anatarajia kujifungua watoto wengine pacha, lakini bado hajabaini jinsia yao.
Anatarajia kufahamu hilo Desemba.
Wanawake hao waliozaliwa Nigeria waliamua kupigwa picha za pamoja wakiwa wajawazito walipofahamu kwmaba dada yao mdogo alikuwa azuru California, jimbo walilokulia. Kwa sasa anaishi Atlanta.
Huo ulikuwa wakati wa kwanza kwao kukutana wakiwa wajawazito na hivyo wakaamua kuwa na kumbukumbu.
"Kwani ni mara ngapi mtapata tena fursa ya kuwa wajawazito kwa pamoja? Ni baraka ambayo lazima tuinakili," Okafor aliambia Yahoo Lifestyle.
Picha zilipigwa na rafiki yao Cynthia Onyejiji.
Dada hao wanatumai kwamba uhusiano wao wa karibu utaigwa na watoto wao.
Wameambia BBC kwamba mama yao alijawa na furaha sana, anamekuwa akisambaza picha hizo kwa jamaa na marafiki.
Lakini kuna kibarua cha kuwasaidia watakapojifungua, wanatarajia kwamba wakwe zao watafika kuwasaidia naye mama yao amsaidia mdogo wao Babalola.
Chanzo - BBC