Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI YA APOLLO YA INDIA YATOA OFA YA MATIBABU KWA WANAMUZIKI WA TANZANIA


Daktari Bingwa wa kutibu bila ya kufanya upasuaji kutoka Hospitali ya Apollo, Dr Sandip Jhala akielezea namna wanavyofanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye kizazi, tezi dume na magonjwa mengine katika mkutano uliowakutanisha Wanaumoja wa Wanamuziki Tanzani (TAMUFO) pamoja na wawakilishi wa Hospitali ya Apollo hapa nchini mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Rais wa TAMUFO, Dkt. Donald Kisanga akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwanamuziki Kasim Salehe Mafanya, akiwa na mwanamuziki wa nyimbo za injili katika mkutano huo.
Viongozi wa TAMUFO na wadau wa muziki wakiwa meza kuu. 
Lina Munisi aliyetolewa uvimbe na Dr.Jhala bila ya kupasuliwa katika Hospilati ya Apollo nchini India akitoa ushuhuda wake kwa wanamuziki.
Mlezi wa TAMUFO, Dk.Juliana Pallangyo, akizungumza kwenye mkutano huo.
Wadau mbalimbali pamoja na wanamuziki wakiwa kwenye mkutano.
Mwanamuziki mkongwe Mzee Makassy akiwa kwenye mkutano huo.
Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stellah Joel, akizungumza kwenye mkutano huo. 

Na Kulwa Mwaibale

Hospitali ya Kimataifa ya Apollo yenye makao makuu yake nchini India, imetoa ofa ya matibabu kwa wanamuziki wa Tanzania.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano baina ya wawakilishili wa Hospitali ya Apollo nchini Tanzania pamoja na wanachama wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Parwez Audax alisema lengo la kutoa ofa hiyo ni kuhakikisha wanamuziki nchini wanakuwa na afya njema.

Audax alisema, baada ya kubaini watu wengi nchini wanasumbuliwa na maradhi hususan ya uvimbe kwenye kizazi kwa wanawake, tezi dume, saratani ya ini pamoja na magonjwa ya mgongo na uti wa mgongo wameamua kutoa ofa ya matibabu kwa gharama nafuu kwa wanamuziki.

"Kwa kuanzia tumeamua kutoa ofa ya gharama nafuu kwenu wanamuziki kwa watakaojiunga na bima ya afya ya Apollo," alisema mwakilishi huyo.

Naye Dr Sandip Jhala ambaye ni miongoni mwa madaktari bingwa wanaotibu bila kufanya  upasuaji wa Hospitali ya Apollo, alisema baada ya kuona watu wengi kutoka nchi za Afrika wanasumbuliwa na uvimbe kwenye kizazi, tezi dume na magonjwa mengine aliamua kuja Afrika kutoa tiba.

"Nilipoona watu wengi kutoka Afrika hususan Tanzania wanakuja kwenye hospitali yetu ya Apollo India kutibiwa niliamua kuja kufanya utafiti kujua ukubwa wa tatizo na kutoa tiba," alisema Jhala.

Dr. Jhala alisema matibabu ya kuondoa uvimbe katika kizazi kwa wanawake bila ya kufanya upasuaji hayahitaji nusu kaputi na mgonjwa hutumia siku mbili tu kukaa hospitali na anakuwa na asilimia 33 mpaka 53 ya kupata mtoto.

Daktari huyo alisema ugonjwa wa tezi dume ambao chanzo chake ni njia ndogo ya kupitisha haja ndogo kubana na kufanya ugumu wa haja ndogo kupita  unatibika kwa muda mfupi.

Dr. Jhala aliwashauri wanamuziki wa Tanzania kujiunga na bima ya afya ya Hospitali ya Apollo ili waweze kupata ofa ya matibabu kwa gharama nafuu watakapokwenda kutibiwa India au hapa nchini.

Rais wa TAMUFO, Dk. Donald Kisanga aliwashukuru wawakilishi hao wa Hospitali ya Apollo nchini kwa ofa hiyo ya matibabu waliyoitoa kwa wanamuziki.

"Tunawashukuru sana kwa ofa mliyotupatia, tutaichangamkia kwa kujiunga na bima yenu mara tutakapokaa nanyi ili mtupe muongozo wa kujisajili," alisema.

Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stellah Joel aliwashukuru Apollo kwa kuwajali wanamuziki wa Tanzania na kusema kwa kuwa wanazo hela watajiunga na mfuko wao wa bima ili waanze kunufaika na ofa waliyowapatia.

Mlezi wa TAMUFO, Dk. Juliana Pallangyo aliwashukuru Apollo kwa ofa waliyowapa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com