Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dkt Vicensia Shule amehudhuria kikao cha kamati ya maadili cha chuo kikuu cha Dar es Salaam na kuwaeleza njia ambazo wanaweza kuzitumia ili kuboresha maadili chuoni hapo.
Katika kikao hicho Dkt.Vicensia amesema kwamba walijadili namna ambayo itaweza kutatua tatizo la rushwa ya ngono lililopo chuoni humo na mpaka sasa hawezi sema muafaka walioufikia kwa sababu yeye aliwasilisha na kuondoka.
Dkt Vicensia alizua mjadala mtandaoni baada ya kudai kwamba rushwa ya ngono imekithiri chuoni humo na kuitwa kufika kwenye kamati ya maadili ya chuo hicho.
Barua ya kamati hiyo iliyotiwa saini ya mwenyekiti Prof Evelyne Mbede inamtaka mhadhiri huyo kufika mbele ya kamati hiso Ijumaa saa tisa "ili kamati iweze kulifanyia kazi swala hili kwa haraka."
Dkt Vicensia Shule alikuwa ameandika kwenye Twitter kwamba alitaka sana kuufikisha ujumbe wake kwa Rais John Magufuli lakini aliwaogopa walinzi wake.
Dkt Magufuli alikuwa amezuru chuo hicho kufungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwalimu. Julius K. Nyerere) jijini Dar es Salaam.
Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati ilijengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na ndiyo maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.
Dkt Shule alitaka kutumia bango kuufikisha ujumbe kwa rais huyo.
Aliandika: "Baba @MagufuliJP umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli."
Alhamisi jioni, aliandika kwenye Twitter kwamba amepigiwa simu na kutakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya UDSM.
"Leo Alhamisi 29 Nov jioni nimepigiwa simu kuitwa kwenye Kamati ya Maadili siku ya Ijumaa 30 Nov mchana. Nasubiri mwaliko rasmi kwa maandishi," aliandika.
"Kwa manusura wa udhalilishaji huu wa kingono, tunakaribia kufika, tutashinda, tutapata ushindi mkubwa!"
Ingawa hakueleza ni rushwa ya aina gani iliyokithiri, katika vyuo vikuu vingine kumekuwepo na tatizo la wahadhiri na wanafunzi kutumia ngono katika kutoa alama katika mitihani.
Aidha, baadhi ya wahadhiri hutuhumiwa kudai ngono kutoka kwa wenzao ndipo wawapandishe vyeo vyuoni.
Tamko lake lilizua mjadala mtandaoni, baadhi wakikubaliana naye na wengine kumwambia angetumia tu ujasiri na kutimiza azma yake.
Mtaalamu wa mawasiliano na mtetezi wa haki za wanawake Bi Maria Sarungi amesema Dkt Shule alipotoa kauli yake, pengine alitatarajia angeukwa mkono na baadhi ya viongozi lakini badala yake ameishia kulaumiwa na kushutumiwa.
CHANZO - BBC
Social Plugin