Siku mbili baada ya kushinda kesi ya kudaiwa kutoa taarifa za uongo na kudanganya kuwa alitekwa, Mwenyekiti wa Mtandao Wa Wanafunzi Nchini (TSNP), Abdul Nondo amejitokeza hadharani na kusema alitekwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Novemba 7, Nondo amesema alitekwa, lakini anamshukuru Mungu na atarudi kuendelea na kumalizia ngwe ya mwisho wa masomo yake.
“Kama Mahakama imeniachia huru ina maana watekaji wangu wapo, naamini Jeshi la Polisi litaendelea na kazi ya kuwasaka watesi hao ili wapatikane.
“Nawashukuru watetezi walionisimamia hadi leo na naahidi kurudi chuo kuendelea tena na masomo yangu kama hapo awali,” amesema Nondo.
Awali Kaimu Mratibu wa Mtandao huo, Deogratius Bwire amewataka polisi kuanza kuwatafuta watu waliohusika na utekaji kutokana na ukweli kwamba mahakama imeweka wazi kwamba upande wa Jamhhri umeshindwa kuthibitisha tuhuma kwamba Nondo alitoa taarifa za uongo kuhusu kutekwa kwake.
Aidha, Bwire pia amezitaka kanuni na sheria ndogo za vyuo zinazoruhusu kusimamishwa kwa wanafunzi wenye kesi mahakamani zifanyiwe marekebisho kwani zinakiuka haki za msingi za kikatiba.
Asha Bani - Mtanzania
Social Plugin