SERIKALI ipo katika hatua ya mwisho kuruhusu bucha za wanyamapori nchini na kutoa siku 30 kwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) kuwasilisha taarifa ya kitaalamu ya utekelezaji wa mpango huo.
Mpango huo ulibainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, wakati alipozungumza na wafanyakazi wa Tawiri.
Hata hivyo, watafiti mbalimbali wa taasisi hiyo, walionyesha wasiwasi kuhusu uanzishwaji wa bucha hizo nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alisema mpango huo unakuja bila kuwa na maandalizi ya kutosha kwa kuwa kunahitajika usimamizi wa hali ya juu.
Alitoa mfano wa nchi kama Afrika Kusini ambayo nyama ya wanyamapori inayouzwa kwa ajili ya kitoweo hupatikana katika mashamba maalumu yaliyoanzishwa na watu binafsi na siyo katika mapori maalumu ama katika mbuga za taifa.
Alisema ingawa sheria inaruhusu watu binafsi kuanzisha mashamba ya wanyamapori, lakini kasi ya utekelezaji hapa nchini imekuwa ndogo tofauti na nchi nyingine ambazo zimeruhusu mabucha ya wanyamapori.
Hata hivyo, kwa upande wa uwindaji wa kitalii pamoja na uwindaji wa kitoweo, wataalamu hao walisema kutokana na uhifadhi endelevu wa wanyamapori ni vyema ukaendelea kwa uratibu maalumu.
Social Plugin