Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAFUNZI AUAWA KWA KUKATWA PANGA MGUUNI

Aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisangura wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, Emmanuel Nyakitare, (15), amefariki baada ya kukatwa mguu kwa panga na mwanafunzi mwenzake wakiwa wanachunga ng’ombe.

Emmanuel alifariki wakati akisubiri matokeo ya mtihani wa darasa la saba, yaliyotangazwa hivi karibuni. 

Chanzo cha tukio ni kugombania eneo la kulisha mifugo baada ya mtuhumiwa, Charles Kaheke (13), mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kisangura kumkata kwa panga marehemu kwa kumtuhumu kulisha mifugo eneo lisilo lake.

Ofisa Tarafa ya Rogoro, Gasper Richard, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 29, mwaka huu, baada ya wanafunzi hao kugombana na baada ya kutenda kosa hilo mtuhumiwa alikwenda shuleni bila mfuko wa madaftari kama ilivyo kawaida, mwalimu wake alipomuuliza kwa nini hakuwa na daftari akamjibu mwalimu kwamba amnunulie ampe.

“Siku ya tukio marehemu alikwenda kuchunga mifugo yao eneo hilo jirani na nyumbani kwa akina Kaheke, (mtuhumiwa) ambaye alipotoka shule kuja kupata chakula cha mchana alimkuta marehemu eneo hilo, katika kuzozana ndipo mmoja alimkata mwenzake kwa panga na kuvuja damu nyingi,” alisema.

Akielezea tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alisema lilitokea Oktoba 29, mwaka huu, kati ya saa 6 na saa 7 mchana, wakati wanafunzi hao wakichunga mifugo, ndipo ulipozuka ugomvi kugombania eneo la malisho, ndipo mtuhumiwa alikasirika na kumkata mguu mwenzake kwa panga, hivyo kuvuja damu nyingi na kusababisha kifo chake.

“Hata hivyo, baada ya kuona amesababisha kifo cha mwenzake alitokomea na kukimbia kwenda kusikojulikana na mpaka sasa haijulikani alipo na marehemu Nyakitare alikuwa akisubiri matokeo ya darasa la saba mwaka huu, baada ya kufanya mtihani,” alisema Babu.

Babu, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Serengeti, alisema baadaye wazazi wa mtuhumiwa walikwenda kwa familia ya marehemu na kuomba msamaha na kuahidiana mambo ambayo hayakuwekwa wazi, hivyo kulimaliza suala hilo bila kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa hatua zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com