Viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo wamefanya ziara kutembelea Shirika lisilo la kiserikali la Rafiki Social Development Organization (Rafiki SDO) kwa ajili ya kujionea shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo kwenye halmashauri hiyo katika kuhakikisha wananchi wenye hali ya chini wanajikwamua kimaisha.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngasa Mboje aliyekuwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Thomas Tukay na maafisa wengine imefanyika leo Ijumaa Novemba 30,2018.
Awali viongozi hao walipokea taarifa ya shughuli zinazofanywa na shirika hilo kisha kukutana na watoto 10 kutoka kata ya Mwakitolyo waliokuwa vibarua katika mgodi wa Mwakitolyo wanaosoma kwa ufadhili wa Rafiki SDO katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija mjini Shinyanga
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mboje alisema lengo la ziara ni kujionea kwa vitendo shughuli zinazofanywa na shirika la Rafiki SDO ikiwa ni sehemu ya kujiridhisha badala ya kupeana taarifa za kwenye makaratasi ili kujenga ushirikiano na uwazi katika utendaji.
“Tunawashukuru sana kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwasaidia wananchi,tunatambua shughuli zenu nzuri za kuwakwamua kiuchumi wananchi”,alisema.
Mboje alitumia fursa kuwataka watendaji wa vijiji na kata kushirikiana na wadau wa maendeleo yakiwemo mashirika kwa lengo ni moja tu kuwatumikia wananchi.
Aliyataka mashirika kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali pale wanapokosa ushirikiano ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO,Gerald Ng’ong’a alizitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kwenye maeneo wanayotekeleza miradi kuwa ni ushirikiano mdogo wa viongozi wa serikali mfano Mtendaji wa kata ya Mwakitolyo hali inayosababisha kushindwa kufikia malengo ya mradi wa kupinga ajira za utotoni.
Aliitaja miradi sita inayotekelezwa na shirika hilo kuwa ni mradi wa kupinga ajira za utotoni,Tulonge afya,Ulinzi wa haki za mtoto na utawala,Kupinga ukatili wa kijinsia,Kupinga mimba na ndoa za utotoni na mradi wa Sauti.
Aidha aliishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa na kwamba ziara hiyo ya viongozi wa halmashauri itakuwa chachu ya mabadiliko zaidi ili kuwainua wananchi kiuchumi.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO,Gerald Ng’ong’a akiwakaribisha viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika ofisi za shirika hilo Mjini Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngasa Mboje akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Thomas Tukay,Kaimu Mganga mkuu wa halmashauri,Bashiri Salum,kaimu Afisa Maendeleo ya jamii,Edmund Ardon na Mratibu wa Ukimwi halmashauri hiyo, Happiness Misael - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO,Gerald Ng’ong’a akizungumza wakati viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga walipotembelea shirika hilo kujionea shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO,Gerald Ng’ong’a akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngasa Mboje akizungumza wakati wa ziara yao kwenye shirika la Rafiki SDO.
Kushoto ni Mratibu wa Ukimwi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Happiness Misael akizungumza wakati ziara hiyo.
Afisa Mradi wa Ulinzi wa mtoto,haki na utawala wa shirika la Rafiki,Tangi Clement akielezea shughuli zinazofanywa na shirika katika maeneo ya afya,elimu,uwezeshaji kiuchumi,ulinzi wa mtoto,haki na utawala na ujasiriamali.
Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia taarifa ya shirika la Rafiki SD wakati Tangi Clement akisoma taarifa kwao.
Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na viongozi wa shirika la Rafiki SDO wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ofisi za Rafiki SDO.
Kijana Chalo Adam ambaye ni miongoni mwa watoto 8 kati ya 10 ambao wamesomea ufundi umeme kwa ufadhili wa shirika la Rafiki katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija akionesha jinsi wanafanya ufundi umeme majumbani wakati viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga walipotembelea chuo hicho kujionea shughuli zinazotekelezwa na Rafiki SDO.
Vijana ambao awali walikuwa vibarua migodini kisha kuchukuliwa na shirika la Rafiki SDO na kusomeshwa katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija kusomea masuala ya umeme wakionesha jinsi wanavyounganisha umeme majumbani.
Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Thomas Tukay akiwapongeza vijana hao kwa ujuzi walioupata kwenye chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija.
Kijana Benjamin Clement akitoa maelezo kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga jinsi wanavyounganisha umeme.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngasa Mboje akiangalia batiki katika darasa la fani ya ushonaji nguo katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi. Wanafunzi wawili wa kike ambao walikuwa wanasaidia mama lishe kwenye mgodi wa Mwakitolyo wamesomeshwa na shirika la Rafiki SDO.
Katikati ni Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii,Edmund Ardon akiangalia nguo zilizotengenezwa na vijana katika Chuo cha Maendeleo ya jamii.
Kijana Jefta Eziel akilishukuru shirika la Rafiki SDO kwa kusomesha watoto/vijana 10 waliokuwa vibarua katika mgodi wa Mwakitolyo na sasa vijana wa kiume 8 wamehitimu mafunzo fani ya umeme na wawili wa kike fani ya ushonaji.
Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija Maria Mkanwa akimweleza jambo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngasa Mboje na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Thomas Tukay walipotembelea chuo hicho kukutana na wanafunzi waliosomeshwa na shirika la Rafiki SDO.Kulia ni Mkurugenzi wa shirika la Rafiki SDO,Gerald Ng'ong'a
Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,viongozi wa shirika la Rafiki SDO na vijana waliosomeshwa na shirika la Rafiki katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog