Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia : MTANGAZAJI MAARUFU WA STAR TV, RFA SAMADU HASSAN AFARIKI DUNIA



Mtangazaji maarufu wa kituo cha Star TV na Radio Free Africa, Samadu Hassan amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake eneo la Miembe Mitatu, jirani na kituo cha Chakechake wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Akizungumza na Mwananchi Digital asubuhi hii, mdogo wa Samadu, Latifa Hassan amesema kaka yake alikuwa akisumbuliwa na kifua kwa zaidi ya wiki moja, kabla ya kufikwa na umauti usiku.

“Samadu alirudi nyumbani kwake jana jioni, akitokea kazini na alikuwa mzima wa afya, japo alikuwa akilalamika kuwa kifua kilikuwa kinamsumbua kwa takriban wiki nzima sasa,” amesema Latifa.

“Tulikuwa na maongezi naye kwa muda na baadaye tukala naye chakula hadi tukamaliza, akatueleza kifua kinamsumbua, tukamshauri pengine twende hospitali usiku huo kupata matibabu akasema angeenda kesho (leo).”

Hata hivyo anasema ilipofika saa sita kasoro usiku, ghafla hali yake ilianza kubadilika na alianguka chini na kuanza kutokwa na mapovu mdomoni.

“Hali hiyo ilitufanya tukimbie kwenda kutafuta gari ili kumuwahisha hospitali, lakini hadi tumepata gari na kurudi ndani tukakuta tayari ameshafariki,” amesema Latifa.

Na  Baraka Samson - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com